Tarehe Mosi Februari huadhimishwa hapa nchini Iran kama kumbukumbu ya kihistoria ya kurejea nchini Imam Khomeini, mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, baada ya karibu miaka 15 ya kuwa uhamishoni.

Imam Khomeini alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Kurejea  Imam Khomeini kulikuwa utangulizi wa harakati isiyo ya kawaida ya watu na matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu, ambayo hayajawahi kutokea katika karne za hivi karibuni.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanachukuliwa kuwa mapinduzi muhimu na makubwa zaidi katika nusu ya pili ya karne ya 20. Kwa hakika ushindi wa mapinduzi hayo, ulikuwa ni utekelezaji wa nia na irada ya taifa kubwa ya kupata uhuru na heshima na kuondoka katika chini ya makucha ya tawala za kibeberu; wakati dunia ilipogawanywa katika pande mbili za Mashariki na Magharibi. Mapinduzi ya watu wa Iran yenye kauli mbiu ya “Hapana kwa Mashariki wala Magharibi” na chini ya uongozi wa Imam Khomeini (RA) yalipata ushindi mnamo 11 Februari 1979.

Kuanzia tarehe Mosi-11 Februari (12 hadi 22 Bahman 1357), siku ya ushindi wa mapinduzi, kulitokea matukio nchini Iran ambayo yalipelekea kubomolewa mfumo fisadi wa kifalme. Siku hizi 10 za hatima ziliharibu mahesabu ya utawala wa kifalme na wafuasi wake, ikiwa ni pamoja na Marekani; kushindwa njama za kuzuia Imam Khomeini kurudi nchini tarehe 12 Bahman, kuundwa serikali ya mpito na Imam Khomeini (RA), tamko la mshikamano wa wafanyakazi wa sekta nyeti kama vile ya mafuta na uasi wa mapinduzi ya watu, kuvunjwa Baraza la Kifalme, kutokuwa na athari kanuni za sheria za kijeshi kwa amri ya Imam na uwepo wa watu mitaani, na utii wa kihistoria wa kundi la wafuasi wa Imam zilikuwa miongoni mwa matukio muhimu zaidi ya hatima yaliyoamua ushindi wa mapinduzi.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kwa uongozi wa Imam Khomeini (RA), hayalinganishwi na mapinduzi yoyote katika nchi zingine katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Kimsingi ni kuwa, ukitoa  Mapinduzi ya Kiislamu, hakuna mapinduzi mengine ambayo yamekuwa na sifa na vipengele vya mapinduzi ya kweli yanayojumuisha imani na maadili yote ya jamii hiyo na ushiriki wa matabaka yote ya kijamii.

Imam Khomeini (RA), ambaye alikuwa akifahamu hali ya kisiasa, kitamaduni, na kijamii ya jamii ya Iran katika mwaka wa kilele cha harakati hiyo na kabla yake, aliona jambo muhimu zaidi la ushindi na siri ya mafanikio kuwa “mageuzi ya Kimungu” ambayo yalikuwa yameundwa katika roho za watu. Katika hali kama hizo; watu walibadilishwa na maneno ya Imam na wakati huo huo, kwa heshima kwa Mwenyezi Mungu, hawakuogopa utawala dhalimu na walisimama dhidi yake kwa ujasiri na ushujaa mkubwa.

Kurejea nchini Imam Khomeini (RA) na ushindi wa mwisho wa Mapinduzi ya Kiislamu uliopatika siku kumi baadaye tangu kurejea kwake ni mambo mawili muhimu katika historia ya kisasa ya Iran. Siku hizi kumi zinazofahamika kama Alfajiri Kumi hazikuwa tu mwanzo na kukamilika harakati ya wananchi dhidi ya utawala dhalimu wa Shah, bali pia mwanzo wa sura mpya katika maisha ya kijamii, kisiasa, na kitamaduni ya taifa la Iran.

Kwa mtazamo wa kihistoria, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliweza kubadilisha taswira ya Iran duniani. Yalitia msukumo mataifa mengine barani Asia, Afrika, na Asia Magharibi, yakionyesha kwamba imani na ufahamu vinaweza kuwa changamoto kwa mataifa makubwa. Harakati nyingi za uhuru baadaye zilijifunza kutoka kwa mfumo wa Iran na kutumia thamani kama vile uhuru, haki, na muqawama katika mapambano yao.

Athari ya Mapinduzi ya Kiislamu bado zinaendelea kuonekana. Mapinduzi haya hayakubadilisha tu muundo wa kisiasa wa nchi, bali pia yaliweka hai roho ya kujiamini, uvumilivu, na ukuaji wa kisayansi katika taifa la Iran. Alfajiri Kumi na siku za kukumbuka ushindi wa mapinduzi ni fursa ya kupitia tena thamani hizi za kimaadilio ili vizazi vipya viweze pia kujua kwamba kilichoifanya Iran ijivunie na kujitegemea ni imani, umoja, na watu wake kupigania malengo na matukufu yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *