
Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi wa michezo, Clemens Fritz, amesema uamuzi huo ulikuwa mgumu, lakini klabu hiyo haikuona matumaini kwamba Steffen angeweza kubadili hali ya timu baada ya kipindi kirefu cha matokeo mabaya.
Fritz amesema wanatafuta kocha mpya kwa umakini mkubwa ili kupata suluhisho bora kwa klabu na kwa sasa wasaidizi Raphael Duarte na Christian Groß wataiongoza timu kwa muda, huku Bremen ikijiandaa kukutana na Freiburg ugenini.
Bremen imemtimua Steffen baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Borussia Mönchengladbach jana Jumamosi, matokeo yaliyopatikana kwa bao la dakika za majeruhi, lakini bado yakiiweka Bremen pointi moja tu juu ya eneo la kushuka daraja. Kwa ujumla, Bremen imeshinda mechi nne tu, sare saba na kupoteza tisa msimu huu, na ilitolewa kwenye mashindano ya Kombe la Ujerumani katika raundi ya kwanza.
Steffen alijiunga na Bremen majira ya kiangazi akitokea Elversberg ya daraja la pili, ambako aliiongoza kutoka daraja la nne hadi karibu kupanda Bundesliga, akirithi nafasi ya Ole Werner, ambaye alifutwa kazi na Bremen baada ya kukataa kuongeza mkataba na klabu hiyo na sasa ni kocha wa Leipzig.