KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuhifadhi mazingira, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeachana na matumizi ya kuni na mkaa katika kuandaa chakula kwa vijana waliopo katika makambi yake nchini.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha taasisi zenye watu wengi zinatumia nishati safi na kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Akizungumza leo Juni 15, 2026 katika Kikosi cha 832 Ruvu JKT mkoani Pwani wakati akifungua mafunzo ya vijana wa Mujibu wa Sheria wanaoshiriki Operesheni Linda Amani, Mabele alisema vikosi vyote vya JKT vinaelekezwa kutumia nishati safi ya kupikia.
Alisema kwa sasa JKT inatumia majiko ya gesi pamoja na mkaa mbadala unaozalishwa ndani ya vikosi kwa kutumia mabaki ya mimea na malighafi nyingine zinazopatikana katika maeneo ya makambi hayo.
“Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia, Jeshi la Kujenga Taifa limeachana na matumizi ya mkaa na kuni katika kuandaa chakula kwa vijana wetu makambini,” alisema.

Mabele alisema hatua hiyo imekuwa muhimu kutokana na idadi kubwa ya vijana wanaopatiwa mafunzo katika makambi ya JKT, akitolea mfano Kikosi cha Ruvu chenye zaidi ya vijana 5,000 wanaoshiriki mafunzo kwa sasa.
Alisema matumizi ya kuni na mkaa kwa idadi hiyo kubwa ya vijana yangesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kuongeza gharama za uendeshaji wa makambi.
“Kwa sasa kuni katika vikosi vya JKT tumezifuta kabisa. Hatutumii kuni wala mkaa wa kawaida. Kinachotumika ni majiko ya gesi na mkaa mbadala tunaoutengeneza wenyewe,” alisema.
Alibainisha kuwa utekelezaji wa mpango huo umewezeshwa kwa ushirikiano wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambao ulitoa mafunzo na vifaa vya kusaidia utengenezaji wa mkaa mbadala pamoja na majiko yake.
Mabele alisema ushirikiano huo utaendelea kupanuliwa katika vikosi vyote vya JKT ili kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanaimarishwa zaidi nchini.
Aliongeza kuwa matumizi ya gesi na mkaa mbadala yamekuwa na manufaa makubwa ikiwamo kupunguza gharama za nishati, kulinda mazingira na kuboresha afya za watumiaji kutokana na kupungua kwa moshi unaotokana na kuni na mkaa wa kawaida.

Aidha, alisema elimu ya matumizi ya nishati safi imejumuishwa katika mafunzo yanayotolewa kwa vijana wa Mujibu wa Sheria na wale wa kujitolea wanaojiunga na JKT.
Alisema vijana hao wanapomaliza mafunzo hubeba maarifa hayo na kuyapeleka katika jamii zao, jambo linalosaidia kueneza matumizi ya nishati safi na kuimarisha utunzaji wa mazingira nchini.
“Tunaamini kupitia vijana hawa, elimu ya matumizi ya nishati mbadala itaendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na kusaidia kufanikisha ajenda ya Serikali ya matumizi ya nishati safi,” alisema.
Serikali imekuwa ikihamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda misitu na kuboresha afya za wananchi, hususan wanawake na watoto ambao huathirika zaidi na moshi unaotokana na matumizi ya nishati zisizo safi.