
Chama kikuu cha kisiasa katika jimbo la kaskazini mwa Ethiopia, TPLF, kimebainisha tena kujitolea kwake kwa mchakato wa amani licha ya mashambulizi. Vile vile, mkuu wa utawala wa mpito katika jimbo hilo, Jenerali Tadesse, ametoa wito wa mazungumzo. Nia ya utulivu inakuja baada ya makabiliano kadhaa kati ya vikosi vya Tigray na jeshi la shirikisho wiki iliyopita. Mashambulizi mawili ya ndege zisizo na rubani pia yalipiga malori ya mizigo kaskazini mwa Tigray.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Addis Ababa, Clothilde Hazard
Kwenye televisheni ya Ethiopia, Jenerali Tadesse ametaka kuuhakikishia umma: “Kujiondoa kwetu kunaonyesha wazi kwamba hatuna nia ya kurudi vitani,” ametangaza, kabla ya kulaani mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na kutetea amani na mazungumzo.
Ujumbe huo ulirudiwa upande mwingine. Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) kimetangaza utayari wake wa kushiriki katika mazungumzo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika (AU) na kuthibitisha tena kujitolea kwake kwa mchakato wa amani uliosainiwa mjini Pretoria, Afria Kusini, mnamo mwaka 2022.
Hata hivyo, pande hizo mbili zilikabiliana katika mapigano huko Tigray wiki hii iliyopita, mapigano makali zaidi tangu mwisho wa vita, kulingana na mtafiti René Le Fort. Lakini anabaini kwamba hakuna dalili kwamba huu ndio utangulizi wa vita kamili, na sababu ya mapigano hayo bado haijulikani, na vile vile mkakati wa serikali ya shirikisho haueleweki.
Waziri Mkuu Abiy Ahmed amesalia kimya na hajatoa maoni yoyote kuhusu mashambulizi ya ndege zisizo na rubani. Kutokuwa na uhakika huku kunasababisha wasiwasi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo. Safari za ndege za Ethiopian Airlines bado hazijaanza tena katika eneo hilo; zimesitishwa kwa siku nne sasa.