Chanzo cha picha, Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4
Makumi ya wanaume wametapeliwa katika mojawapo ya kashfa ya ulaghai wa ndoa nchini India. Wanaume hao waliokuwa wamesafiri hadi mji wa Dewas katika jimbo la Madhya Pradesh wakiwa na matumaini ya kufunga ndoa waligundua, baada ya kusubiri kwa saa kadhaa, kwamba walikuwa waathirika wa mtandao uliopangwa waulaghai.
Asubuhi ya Mei 24, hekalu la Mata Tekri mjini Dewas ilikuwa imepambwa tayari kwa sherehe kubwa ya harusi. Wanaume kutoka miji na vijiji mbalimbali, baadhi yao wakiwa na jamaa zao, wengine wakiwa na magari ya kukodi, walikuwa wamefika kwenye ukumbi huo. Wengi wao walikuwa wamevalia mavazi ya harusi, tayari kwa moja ya siku muhimu zaidi maishani mwao.
Waliambiwa kwamba wangefunga ndoa ndani ya saa 24 zijazo. Lakini maharusi hawakujitokeza na hivyo ndivyo halfla hiyo ilivyotibuka.
Kwa mujibu wa polisi, kilichotokea huko Dewas ni ulaghai ulioenea uliojificha kama “ndoa ya pamoja”; mpango ambapo wanaume wanaotafuta wake walitozwa kiasi kikubwa cha pesa kwa ahadi za uwongo.
Naibu Kamishna wa Polisi wa Dewas, Jivirsen Bhadriya, alisema uchunguzi umebaini kuwa watu wengi wamekuwa wakilengwa katika kashfa hiyo. Watu wawili wamekamatwa kufikia sasa na uchunguzi unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata washtakiwa wengine katika kesi hiyo.
Mtandao wa utapeli
Kulingana na polisi na waathiriwa, kashfa hiyo ilipangwa kwa uangalifu. Wanachama wa mtandao huo kwanza waliwatambua wanaume wanaotafuta wake na kisha kuwafahamisha kwamba wasichana wanaoishi katika kituo cha kidini katika jiji la Indore walikuwa tayari kwa ndoa.
Katika hatua iliyofuata, fedha zilikusanywa kutoka kwa waliowasilisha maombi kwa kisingizio cha usajili, kuandaa hati, na kukamilisha taratibu za kisheria. Hatua zote zilifanywa kupitia simu za rununu na mtandao.
Ili kupata imani zaidi, picha za wasichana hao zilitumwa kwa familia; picha hizo baadaye zilibainika kuwa zilikusanywa kutoka kwenye mitandao ya kijamii na hazikuwa na uhusiano wowote na tukio hilo.
waathiriwa wa ome pia wanasema kwamba jina la waziri mkuu wa serikali lilitumika kunadi mpango huo. Waliambiwa kwamba maafisa wa serikali wangehudhuria sherehe hiyo na kwamba msaada maalum wa kifedha ungetolewa kwa wanandoa hao.
Chanzo cha picha, SAMEER KHAN
Mmoja wa vijana ambaye alikuwa mwathirika wa tukio hilo anasema: “Tuliambiwa kwamba wasichana walikuwa katika hali nzuri sana na tayari kuolewa. Kila kitu kilionekana kuwa sawa kiasi kwamba hatukuwa na sababu ya kuwatilia shaka.”
Anaeleza kuwa alipoomba kukutana na msichana aliyemchagua, aliambiwa kuwa kwa kuwa wasichana hao walikuwa wakikaa kwenye makazi ya kidini, mkutano wa kabla ya harusi haukuwezekana. Badala yake, alihakikishiwa kwamba pande zote zitapata fursa ya kukutana na kuzungumza siku moja kabla ya hafla ya ndoa.
Siku ambayo wachumba walijitokeza na maharusi wakatoweka
Mmoja wa walalamishi alisema alikuwa amesafiri hadi Dewas akiwa na jamaa zake tisa kuhudhuria sherehe hiyo. Walipofika, walipata makumi ya wanaume wengine wakiwa na matumaini na matarajio yayo hayo.
Kulingana na yeye, takribani wapambe 42 walikuwa wamekusanyika katika ukumbi huo. Wengi wao walikuwa na umri wa miaka 40, na kulikuwa na wanaume wenye umri wa miaka 60 miongoni mwao.
Vikas Meena, mwathiriwa mwingine, anasema alilipa Rupia 25,000 za usajili na kukamilisha mchakato wa ndoa.
”Tuliambiwa tutaoa wasichana kutoka katika kituo cha watoto yatima,” anasema. “Walitutumia picha hizo na kila kitu kilionekana kuwa halisi. Baadaye tuligundua kuwa picha hizo zote zilikuwa zimetolewa kwenye mitandao ya kijamii.”
Miongoni mwa waliohudhuria ni Om Prakash Prajapati, mwanamume aliyemchagua mke wake mtarajiwa baada ya kuona picha hizo na kuhudhuria sherehe hiyo akiwa na matumaini makubwa.
Anasema waandalizi hao walitoa hata maelekezo kuhusu mavazi, sherehe na matambiko kabla ya harusi, huku wakizitaka familia kutofanya sherehe zozote kabla ya kuhudhuria harusi hiyo, kwani shughulu zote zingefanyika katika ukumbi mmoja.
Saa kadhaa za kusubiri na mashaka
Familia hizo zilifika hekaluni mapema asubuhi, huku waandalizi wakiwahakikishia mara kwa mara kwamba maharusi walikuwa njiani na wangewasili muda mfupi ujao kutoka Indore.
Lakini kadiri muda ulivyopita, hakukuwa na dalili zozote za maharusi. Adhuhuri iligeuka jioni, jioni ikawa usiku, na mwishowe waliokuwepo waligundua kuwa walikuwa wamedanganywa. Zogo likazuka na hapo ndipo maafisa wa polisi walifahamishwa wakaja eneo la tukio.
“Katikati ya purukushani hizo, mmoja wa waandaaji wa tukio hilo alidai kuwa yeye pia ni mhanga wa tukio hilo, alidai kuwa kaka yake ndiye mhusika mkuu wa mpango huo na kila senti anayoipata alimpelekea kaka yake, na yeye pia alidanganywa.
Uchunguzi wa polisi na hatima ya kesi
Baada ya kupokea malalamiko mengi, polisi walifungua kesi rasmi.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba kiwango tofauti cha pesa kilipokelewa kutoka kwa watu binafsi, baada ya kutumiwa picha za uwongo, na ahadi nyingi za uwongo zilitolewa kuhusu ndoa, usaidizi wa kifedha, na manufaa mengine.
Polisi wamemkamata mmoja wa washukiwa wakuu, na msako wa kuwatafuta watu wengine wanaohusishwa na mtandao huu unaendelea.
Wakati huohuo, waathiriwa wa kashfa hiyo wamerejea makwao wakiwa na machungu, aibu na hisia ya kukata tamaa.
Mmoja wao, kijana mwenye umri wa miaka 22, anasema kwamba ana wasiwasi zaidi kuhusu maoni ya wale wanaomzunguka na maisha yake ya baadaye.
Anasema: “Nimewaomba wanaofahamu tukio hili wasichapishe suala hilo. Lakini wakati huo huo nimeamua kufuatilia kesi hii hadi mwisho. Waliocheza hisia na imani ya wananchi lazima wawajibishwe kwa matendo yao.”
Chanzo cha picha, SAMEER KHAN