Aboutwalib Mshery, Khomein Abubakar na sasa Hussein Masalanga, hawa wote wanasubiri mbele ya Djigui Diarra ambaye ameweka mizizi yake golini pale Yanga tangu alipotua Agosti 2021 akitokea Stade Malien.

Kule Simba baada ya Mousa Camara kuumia ambaye alikuwa kipa namba moja, mikoba ikaangukia kwa Yakoub Suleiman, kwa bahati mbaya naye akaumia. Jukumu akabeba Hussein Abel.

Abel ambaye huu ni msimu wake wa tatu ndani ya Simba aliyojiunga nayo akitokea KMC, ilionekana ni wakati wake kuaminiwa, lakini ikawa tofauti. Alidaka mechi nne pekee zikiwamo tatu za Kombe la Mapinduzi 2026 na moja Ligi Kuu Bara, kabla ya kuletwa kipa raia wa Niger, Djibrilla Kassali aliyechukua nafasi ya Camara.

Kabla ya hapo, Simba ilikuwa na Ally Salim ambaye kudaka kwake hadi kipa namba moja aumie, kuwa na adhabu au sababu nyingine tofauti inayomfanya ashindwe kucheza. Kwa kifupi kipa wa kigeni hapo ndiye namba moja tangu enzi za Ayoub Lakred, Camara na sasa Kassali.

Singida Black Stars wakati ambao Amas Obasogie raia wa Nigeria akikosekana, Metacha Mnata anakaa langoni kulinda nyavu zisitikiswe. Amefanya hivyo michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 na kimataifa.

Kipa wa Azam FC, Zuber Foba. Picha na Mtandao

Ukija viunga vya Chamazi, pale ndio kuna balaa. Kocha Florent Ibenge alichofanya ni kumuamini kijana mdogo Zuber Foba mbele ya wazoefu Issa Fofana na Aishi Manula, ingawa huwa anawapa mechi tofauti tofauti kulingana na mipango yake.

Foba kutoka akademi ya Azam, msimu huu ametoboa na ndiye kipa aliyedaka mechi nyingi zaidi kikosni hapo kupitia mashindano mbalimbali kabla ya jana kukabiliana na Nairobi United katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kabla ya jana Azam kucheza dhidi ya Nairobi United, Foba alidaka mechi tisa kati ya 21 ilizocheza Azam msimu huu kuanzia ile ya kirafiki dhidi ya Mbeya City kabla ya kuanza msimu.

Foba ambaye alidaka mechi hiyo ambayo Azam ilishinda mabao 2-0 pale jijini Mbeya, imemfanya kipa huyo hadi sasa kuwa na clean sheet tano, akiruhusu nyavu kutikiswa katika mechi nne kati ya tisa.

Katika kuonesha Ibenge ana imani kubwa na Foba, hachagui mechi za kumpa, kwani tayari amempanga kudaka dhidi ya vigogo kama Wydad katika Kombe la Shirikisho Afrika na Simba ndani ya Ligi Kuu Bara.

Katika mechi dhidi ya Wydad, Foba aliruhusu bao Azam ikichapwa 1-0, lakini mbele ya Simba akakaza, akaondoka na clean sheet waliposhinda 2-0.

Kabla ya mechi ya jana, takwimu zinaonesha Foba amedaka zaidi katika Kombe la Shirikisho kuliko mashindano mengine kwani amekaa langoni mara sita kati ya saba, huku Ligi Kuu akidaka mbili na kirafiki moja.

Kwa upande Aishi Manula aliyerejea kikosini hapo msimu huu akitokea Simba alipokaa takribani mwaka mzima bila kucheza, ametamba upande wa Kombe la Mapinduzi alipodaka mechi zote tano ilizocheza Azam iliyopoteza fainali kwa penalti 5-4 dhidi ya Yanga. Pia amedaka mechi tatu za Ligi Kuu Bara.

Kipa wa Azam FC, Issa Fofana . Picha na Mtandao

Naye Fofana, kipa raia wa Ivory Coast ambaye ujio wake pale Azam ilionekana anakwenda kutawala kutokana na kufahamiana vizuri na Ibenge, yeye ana mechi chache zaidi ambazo ni nne, tatu Ligi Kuu na moja Kombe la Shirikisho.

Sio Azam tu, Foba alikwenda Afcon 2025, baada ya Yakoub kuumia, akachukua mikoba, naye akaumia, akamalizia Masalanga wakati Taifa Stars ikiishia 16 bora.

Wakati Foba akiaminiwa na Ibenge, hali imekuwa tofauti kwa timu zingine zenye makipa wa kigeni kati ya zile zinazoiwakilisha nchi kimataifa kwa maana ya Yanga, Simba na Singida Black Stars.

Mshery na Khomein wamekuwa wakisubiri mbele ya Diarra na sasa Masalanga ametua naye hali ileile.

Diarra anapokuwa mzima kiafya au hana tatizo lolote linalomfanya akosekane uwanjani, basi atadaka. Hiyo imetokea tangu atue Yanga na msimu huu ameendeleza hilo.

Kwa bahati nzuri, licha ya Diarra kuaminiwa zaidi, lakini hata Mshery na Khomein wakipewa nafasi wanafanya vizuri.

Msimu huu, Mshery amedaka mechi saba za mashindano kati ya 21, huku Diarra akikaa langoni mara 14. Khomein bado na baada ya kuumia, ametolewa kwenye mfumo, nafasi yake ameingia Masalanga aliyetua dirisha dogo msimu huu.

Mshery ndiye alikuwa kipa namba moja wakati Yanga ikibeba Kombe la Mapinduzi 2026 akicheza mechi zote nne, wakati huo Diarra yupo Morocco akishiriki Afcon 2025 akiitumikia Mali.

Ndani ya Simba, Abel amedaka mechi nne za Mapinduzi na moja Ligi Kuu, ikaonekana kimataifa lazima nguvu iongezwe kufuatia kuumia kwa Camara na Yakoub, akasajiliwa Kassali ambaye hatua ya makundi amedaka mechi ya ugenini dhidi ya Esperance ambayo Simba ilichapwa 1-0, jana pia alitarajiwa kukaa langoni timu hizo ziliporudiana Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Leo hii Foba ameaminiwa na Ibenge, kisha naye hajamuangusha, anafanya kweli kulinda milingoti miwili, huku mabosi wa Azam wakikubaliana na hayo yote yanayofanywa na benchi la ufundi. Hili ni somo kwa klabu zingine, kuwaamini makipa wazawa mbele ya wageni.

Akizungumzia uamuzi wa kutoa nafasi kwa kila kipa ndani ya Azam, Ibenge amesema: “Katika kikosi changu kila mchezaji ninamuamini na nikimpa nafasi anafanya vizuri, nawapongeza wote kwa kile wanachokifanya ndani ya uwanja.”

Kipa wa Azam FC, Zuber Foba. Picha na Mtandao

AZAM (mechi 21)

Zuber Foba: 9 (Ligi 2, Kimataifa 6, Kirafiki 1)

Aishi Manula: 8 (Ligi 3, Mapinduzi 5)

Issa Fofana: 4 (Ligi 3, Kimataifa 1)

YANGA (mechi 21)

Aboutwalib Mshery: 7 (Ligi 3, Mapinduzi 4)

Djigui Diarra: 14 (Ligi 5, Kimataifa 8, Ngao ya Jamii 1)

SIMBA (mechi 18)

Mouss Camara: 2 (Ngao ya Jamii 1, Kimataifa 1)

Yakoub Suleiman: 10 (Ligi 5, Kimataifa 5)

Hussein Abel: 4 (Mapinduzi 3, Ligi 1)

Djibrilla Kassali: 3 (Ligi 1, Kimataifa 2)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *