
Morogoro. Operesheni maalumu ya Jeshi la Polisi mkoani Morogoro imeibua mtandao mpana wa uhalifu baada ya kukamata watuhumiwa 124 kwa makosa mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya, pombe haramu, mauaji na makosa ya usalama barabarani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo amesema operesheni hiyo iliyodumu kwa siku 27, kuanzia Mei 15 hadi Juni 10 mwaka huu, ililenga kukabiliana na kuzuia na kutanzua matukio ya uhalifu, ikiwemo dawa za kulevya, ujangili na makosa ya usalama barabarani.
Amesema katika operesheni hiyo, polisi wamekamata kilo 69.9 za bangi, bunda 83 za mirungi, lita 185.5 za gongo na chupa 20 za Smart Gin bandia.
Kwa mujibu wa Kamanda Kantimbo, jumla ya watu 124 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na pombe haramu, ambazo zimeendelea kuwa tishio kwa afya, usalama na ustawi wa jamii.
Katika matukio ya jinai, polisi wanamshikilia mkazi wa Negelo, Paul Gembe (20) maarufu “Sinenepi”, kwa tuhuma za kumuua Kitu Bayayi Geleshi (22) katika Kijiji cha Mziha, Tarafa ya Turiani, Wilaya ya Mvomero.
Tukio hilo lilitokea Juni 8 mwaka huu na chanzo kinadaiwa kuwa ugomvi uliozuka kati ya wawili hao kabla ya marehemu kushambuliwa kwa kitu butu na kufariki dunia, katika mazingira yanayohusishwa na ulevi wa kupindukia.
Katika kukabiliana na uhalifu dhidi ya maliasili, Kamanda Kantimbo amesema watu 42 wamekamatwa kwa tuhuma za uwindaji haramu sambamba na vipande 42 vya nyama inayodaiwa kupatikana kupitia shughuli hizo.
Kwa upande wa usalama barabarani, madereva 24 wamechukuliwa hatua kwa kukiuka sheria, kati yao leseni tisa zimesimamishwa na wengine kupelekwa katika mafunzo maalumu ya udereva ili kuongeza uelewa wa sheria na kanuni za usafirishaji.
Kantimbo amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, vyombo vingine vya usalama na wananchi waliotoa taarifa zilizosaidia kukamata watuhumiwa na kudhibiti uhalifu.
Ameongeza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini mitandao mingine ya uhalifu, huku watuhumiwa wote wakitarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa za uhalifu, ili kuimarisha usalama wa jamii na mali zao.