Marekani. Rapa mwenye ushawishi zaidi duniani kutokea Marekani, Kendrick Lamar ameweka rekodi kwenye tuzo za Grammy za 68, baada ya kushinda vipengele vitano na kukaa kileleni kama rapa mwenye tuzo nyingi zaidi za Grammy duniani.
Hafla ya ugawaji wa tuzo hizo imefanyika usiku wa kuamkia leo Februari 2, 2026, katika jiji la Los Angeles na kumfanya rapa huyo kufikia jumla ya tuzo hizo 27. Akimpindua Jay Z aliyekuwa akishikiria rekodi ya rapa mwenye tuzo hizo nyingi zaidi akiwa na jumla ya Grammy 25.
Kendrick Lamar ambaye alikuwa akiwania tuzo 9 za Grammy. Akiwa msanii aliyewania vipengele vingi zaidi mwaka huu, amefanikiwa kurudi nyumbani na mzigo wa tuzo tano ambazo ni Best Rap Album (GNX), Best Rap Song, Best Melodic Rap Performance, Best Rap Performance (with Clipse) na Record Of The Year.
Hivyo zimemfanya kufikisha jumla ya tuzo 27 na kuwa rapa mwenye tuzo nyingi katika historia ya Grammy.
Sambamba na hilo, Lamar ameweka rekodi ya kuwa rapa aliyeshinda kipengele cha Record of The Year, mara mbili baada ya kushinda kipengele hicho kwa miaka miwili mfululizo 2025 na 2026.
Akizungumza wakati wa kupokea tuzo hiyo katika ukumbi wa Crypto.com Arena, Los Angeles, Lamar aliwapongeza wasanii wenzake walioteuliwa. Huku akiita ushindi wake wa kihistoria kuwa “Hip Hop kama kawaida”.
“Nahisi sio mzuri sana katika kujisifia. Lakini ninaelezea yote kupitia muziki, Nimekuwa nikisema mara kwa mara hip hop itaendelea kuwepo. Tutakuwa hapa tukiwa tumevaa vizuri tukiwa na watu wetu na utamaduni wetu,” amesema Kendrick Lamar.
Ushindi huo wa tuzo tano za Grammy usiku wa kuamkia leo unamfanya Lamar kuungana na Steve Wonder wakiwa wasanii pekee kuwahi kushinda tuzo tano kwa kila mwaka ndani miaka miwili mfululizo. Utakumbuka pia mwaka 2025 Kendrick alishinda tuzo tano za Grammy.
Washindi wengine
Pharrell Williams ametunukiwa tuzo ya la Dr. Dre Global Impact. Tuzo hii inatambua mafanikio yake ya muziki, uvumbuzi wa ujasiriamali, na ushawishi wa kitamaduni wa kimataifa. Ushindi huo ni tafsiri kuwa ushawishi wake sio tu kwenye tasnia ya muziki pekee.
Msanii anayetarajiwa kuwa kinara Headliner wa Super Bowl Half Time Show 2026. Bad Bunny ameibuka mshindi wa tuzo tatu za Grammy. Vipengele alivyoshinda ni Album of the year “DeBÍ TiRAR MáS FOToS”, Best global music performance: “EoO”, Best música urbana album: “DeBÍ TiRAR MáS FOToS” ushindi huo unamfanya kuwa msanii wa pili baada ya Kendrick aliyenyakua tuzo nyingi usiku huo.
Aidha, Mwanamuziki kutokea Marekani Chris Brown ambaye mashabiki wengi walikuwa na matumaini huenda mwaka huu angeibuka mshindi wa tuzo hizo, baada ya kutangazwa kuwania vipengele viwili ameondika mikono mitupu.
Breezy alikuwa anawania tuzo ya Best R&B Performance kupitia wimbo wake wa It Depends. Tuzo ambayo imekwenda kwa Kehlani na wimbo wake wa Folded. Kipengele kingine alichopoteza ni Best R&B Song kupitia wimbo huo huo wa It Depends, lakini tuzo ikaenda tena kwa Kehlani na ngoma yake ya Folded.
Tuzo za Grammy 2026 zimeendelea kutambua vipaji vya wanamuziki kutokea Afrika, ambapo gwiji wa muziki kutokea Nigeria, marehemu Fela Kuti ametunukiwa tuzo ya heshima ya Lifetime Archievement Awards. Utambuzi huo unamfanya Fela kuwa msanii wa kwanza wa Kiafrika kutunukiwa Tuzo hiyo kutoka Grammys.
Watoto wake Fela Kuti Yeni, Kunle, Shalewa na Femi Kuti walikubali kupokea tuzo hiyo kwa heshima ya baba yao. “Nina hakika baba yangu anatabasamu juu yetu,” Yeni alisema katika hotuba ya kupokea tuzo hiyo.
Hata hivyo, staa wa Afrika Kusini, Tyla kwa mara nyingine tena ameibuka mshindi wa tuzo ya Grammy katika kipengele cha Best African Performance kupitia wimbo wake wa PUSH 2 START.
Tyla ameibuka mshindi wa tuzo hiyo mbele ya wababe wa muziki Afrika aliokuwa akichuana nao ambao ni Burna Boy, Davido, Omah Lay, Eddy Kenzo, Ayra Starr na Wizkid. na kumfanya kuwa msanii pekee tokea Afrika kushinda Grammy usiku huo.
Hata hivyo, ukurasa wa Instagram wa tuzo za Grammy umepokea maoni mengi hasi, kutoka kwa mashabiki walioamini Davido alifaa kutangazwa mshindi katika usiku huo.
Hilo limetokea mara baada ya Tyla kutoka Afrika Kusini kutangazwa kama mshindi wa Tuzo ya Best African Performance kupitia wimbo wake wa PUSH 2 START.
Katika picha za Tyla zilizochapishwa kwenye page ya GRAMMY comment nyingi zimelaani na kupinga ushindi huo. Huku wengi wakisema Davido ndiye alistahili kupewa tuzo hiyo kupitia wimbo wake wa WITH YOU aliomshirikisha Omah Lay.
Burna Boy, Davido, Ayra Starr na Eddy Kenzo ni miongoni mwa wakali wa Afrika walioondoka mikono mitupu kwenye hafla ya ugawaji wa tuzo za Grammy.
Burna Boy alikuwa akiwania tuzo ya Best Global Music Album kupitia album yake ya No Sign Of Weakness ambapo tuzo imekwenda kwa Wabrazil Caetano Veloso na Maria Bethãnia kupitia Album yao ya Caetano e Bethaânia Ao Vivo.