Mapema mwezi Januari, maandamano yaliyochochewa na matatizo ya kiuchumi yalizuka nchini Iran. Lakini pia hali ya kutoridhika kisiasa na shinikizo la mataifa ya kigeni kwa pamoja vilisababisha moja ya changamoto kubwa zaidi za ndani ambazo uongozi wa Iran umekabiliana nazo kwa miaka mingi.
Machafuko hayo ya karibuni yalisababisha msuguano mkali wa kikanda, wakati Rais Donald Trump akiamuru jeshi kubwa la Marekani kupelekwa Mashariki ya Kati na kuionya Iran kuzuia mpango wake wa nyuklia na utengenezaji wa makombora.
Wakati wa maandamano hayo, inasemekana China ilisaidia mamlaka ya Iran kukata mawasiliano nchini kote.
Na Januari 31, huku mvutano ukiwa umefika kileleni, vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti kwamba taifa hilo linapanga kufanya luteka ya pamoja ya majeshi ya majini na China na Urusi katikati ya Februari kaskazini mwa Bahari ya Hindi. Tangazo hilo lilifuatiwa na kuongezeka kwa madai ambayo hayajathibitishwa ya mtandaoni kwamba China ilikuwa ikiipatia Iran msaada wa kijeshi, pamoja na uvumi kuhusu iwapo serikali ya China ingeingilia kati makabiliano ya kijeshi ya Marekani.
Iran yaimarisha uhusiano na China
Kwa miaka kadhaa China imekuwa mshirika muhimu wa Iran katika maeneo ya uchumi na diplomasia, kuipatia msaada mkubwa katikati ya vikwazo vikali vya Marekani vinavyoikabili Tehran ambayo pia ipo kwenye orodha mbaya ya Kikosi Kazi cha Kifedha. Vizuizi hivi vimepunguza uwezo wa Iran kufikia mfumo wa kifedha wa kimataifa na kuifanya kuitegemea China kwa biashara na uungwaji mkono wa kisiasa.
Na uhusiano huo uliimarika kwa kiwango kikubwa lakini zaidi kwenye eneo la usalama tangu vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel mwezi Juni 2025 Na miezi michache baadae, ilielezwa kwamba Iran na China wametanua makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama yaliyolenga kuboresha mabadilishano ya taarifa za intelijensia na uratibu dhidi ya vitisho kutoka nje.
Hata hivyo, mchambuzi wa msuala ya Mashariki ya Kati kwenye taasisi ya Masomo ya Kimkakati – SWP- cha mjini Berlin Hamidreza Azizi ametahadharisha dhidi ya namna Beijing inavyojihusisha na kuitetea serikali ya Iran. Amesema namna China inavyojiingiza nchini Iran pamoja na eneo la Mashariki ya Kati kwa kiasi kikubwa bado unasalia kuwa wa kivitendo zaidi na uwezekano ni mdogo kwa China kuisaidia Iran ikiwa atavamiwa na Marekani, kama ambavyo haikujitokeza kwenye vita hivyo ya siku 12.
Uhusiano wa Iran na China kimsingi unaimarishwa na makabiliano na Washington. Wakati vikwazo vya Marekani vikiisogeza Tehran kwa China, wamezuia uwekezaji wa China na kupunguza uwezo wa China kupanua wigo wake wa kiuchumi nchini Iran. Na kulingana na Azizi, wakati China ikitamani ukanda huo ubakie salama ili kulinda maslahi yake mapana ya kiuchumi na nishati, hiyo haimaanishi kwamba itakwenda nje ya mipaka yake ili tu kuitetea serikali ya Iran.
China, Iran, na “Ushirikiano wa Kimkakatiā
Nchini Marekani, ushirikiano kati ya Iran na China mara nyingi hutajwa kama sehemu ya kile ambacho kimeonyeshwa kama “Ushirikiano wa Kimkakati.” Neno hilo linarejelea kuimarika kwa uwiano wa kimkakati, kijeshi na kiuchumi kati ya China, Urusi, Iran na Korea Kaskazini – wenye lengo la kupinga utaratibu wa kimataifa unaoongozwa na Marekani.
Maafisa wa Ulaya na NATO pia wamebaini muunganiko huu. Mkuu wa NATO Mark Rutte, akizungumza katika mkutano huo katika Bunge la Ulaya mnamo Januari 26, alisema, “Ni jambo lisilopingika kwamba, tunavyozungumza, Urusi, China, Korea Kaskazini na Iran zinakaribiana zaidi na zaidi,” na kuongeza kuwa wakati ushirikiano “bado haujaundwa vizuri,” nchi hizi zinazidi kuwa tayari kupinga ushawishi wa Magharibi.