Wanavijiji katika eneo hilo wamelazimika kuburuta mizoga ya mifugo yao hadi mashamba ya mbali ili kuiteketeza, ili kuzuia harufu kali na fisi wanaotafuna mizoga kuyakaribia makazi yao.
Kaunti ya Mandera, iliyo mpakani mwa Kenya, Ethiopia na Somalia, haijapata mvua tangu mwezi Mei na sasa iko kwenye hatari ya dharura kamili ya uhabara wa maji.
Bishar Maalim Mohammed, mwenye umri wa miaka 60, mkazi wa kijiji cha Tawakal, aliliambia shirika la habari la AFP, “Nimepoteza ng’ombe na mbuzi wangu wote, nami nimewateketeza hapa,”.
Katika kijiji chake, ambako wengi ni wafugaji wanaotegemea sana mifugo yao, fahali pekee aliyebaki hawezi tena kusimama.
Amelala sehemu hiyo hiyo kwa karibu wiki moja, akiwa amepungukiwa sana na maji mwilini huku mifupa ikijitokeza nje ya ngozi yake, naye mmiliki wake akitazama bila msaada wowote.
Kukauka kwa vyanzo vya maji
Katika mji wa karibu wa Banissa, bwawa la maji lililokuwa na ujazo wa mita elfu 60,000 za maji sasa limekauka, na kuacha eneo kame ambalo watoto wameligeuza kuwa uwanja wa michezo.
Makundi ya mbuzi, ng’ombe na ngamia sasa hulazimika kutembea hadi kilomita 30 kufika kwenye bwawa la karibu zaidi katika kijiji cha Lulis, wakigombania maji machache yaliyosalia ambayo maafisa wanayafungulia kwa mgao, na huenda yakaisha ndani ya wiki mbili zijazo.
Zaidi ya watu milioni mbili katika kaunti 23 nchini Kenya wanakabiliwa na hali inayozidi kuwa mbaya ya uhaba wa chakula baada ya mvua fupi za Oktoba hadi Desemba kukosa kunyesha, huku kiwango cha mvua kikiwa chini kwa theluthi mbili ya wastani.
Mtandao wa Mifumo ya Tahadhari ya Mapema ya Njaa hivi karibuni ulisema kuwa watu milioni 20 hadi 25 nchini Kenya, Somalia na Ethiopia wanahitaji msaada wa kibinadamu wa chakula, zaidi ya nusu yao kutokana na ukame. Maalim Mohammed ana hofu kwamba “watoto wao ndio wanaofuata kufa.”
Utapiamlo waongezeka kwa kasi
Katika hospitali kuu ya Banissa, ongezeko la watoto waliodhoofika vibaya kwa utapiamlo — baadhi yao wakitoka nchi jirani ya Ethiopia — limelemea wodi ya watoto.
Khalid Ahmed Wethow, mtaalamu wa lishe hospitalini humo, anasema, “Watoto hawapati lishe ya kutosha kutokana na ukame huuwalitegemea maziwa ya ngamia na mbuzi, lakini sasa hakuna maziwa kabisa.”
Hospitali hiyo, inayohudumia takriban watu 200,000, hutegemea michango kutoka kwa mashirika kama Mpango wa Chakula Duniani (WFP), lakini kutokana na nchi za Magharibi kupunguza bajeti za misaada katika mwaka uliopita, haijapokea vifaa vyovyote kwa kipindi cha miezi sita.
Serikali na mashirika yaingilia kati
Serikali ya Kenya na mashirika ya misaada kama Msalaba Mwekundu yameongeza juhudi za kusafirisha maji kwa malori, kutoa msaada wa chakula na fedha taslimu, lakini yanasema hayawezi kuendana na mahitaji yanayoongezeka.
Katika kijiji cha karibu cha Jabi Bar, idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika shule ya karibu imepungua kwa zaidi ya nusu.
Mwalimu mkuu Ali Haji Shabure aliiambia AFP kuwa “wanafunzi 99 pekee ndio waliobaki shuleni, kwa sababu wengi wao wameondoka pamoja na wazazi wao.”
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Bishar Mohamed, anasema walijaribu kukimbia kutafuta maeneo bora lakini walishindwa.
Alisafiri zaidi ya kilomita 150 akiwa na kundi lake la mbuzi 170 akitafuta malisho, lakini takriban 100 walikufa njiani na waliobaki walikufa baada ya kurejea nyumbani katika kijiji cha Hawara. Mvua zinazofuata — iwapo zitanyesha — hazitarajiwi kabla ya mwezi Aprili.