Raundi ya nne ya hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika 2025/2026 ilikamilika jana Jumapili, Februari Mosi, 2026 kwa michezo mbalimbali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa katika viwanja na miji tofauti Afrika.
Timu nne za Tanzania zilikuwa kibaruani katika mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambazo ni Yanga na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam na Singida Black Stars katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Matokeo ya mechi hizo yameziacha timu hizo katika hali ya mtego kwani tatu zinalazimika kupata matokeo mazuri katika mechi zao zilizobakia na moja imeaga rasmi mashindano hayo na ifuatayo ni tathmini ya hali ya mambo ilivyo kwa wawakilishi hao wa Tanzania.
Winga wa Simba, Libasse Gueye akijaribu kumpita beki wa Esperance katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo imemalizika kwa sare ya mabao 2-2. Picha na Simba
Ndoto ya Simba kufanya maajabu ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kupoteza mechi tatu za mwanzo za hatua ya makundi, ilizimika rasmi jana baada ya kutoka sare.
Matokeo hayo yameifanya Simba iage rasmi mashindano hayo kwa vile haitoweza kufikia pointi nane ambazo Stade Malien inayoongoza kundi D inazo kwa sasa lakini hata ikishinda mechi mbili zilizobakia kwake, Simba haitoweza kumaliza katika nafasi ya pili kwa vile itaathirika na matokeo ya mchezo baina ya Esperance na Petro Luanda.
Timu yoyote itakayoshinda mechi hiyo, itafikisha pointi ambazo Simba haitoweza kuzifikia na zikitoka sare, Esperance itafuzu kwa vile hata ikipoteza echi ya mwisho na Simba ikashinda mechi zake, Esperance itafuzu kwa kubebwa na kanuni ya kupata matokeo mazuri kwenye mechi mbili baina yao.
Kwa sasa, Stade Malien inaongoza ikiwa na pointi nane, Esperance inafuatia ikiwa na pointi sita, Petro ina pointi tano na Simba ina pointi moja.
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, akiwatoka wachezaji wa Al Ahly, katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 Jumamosi Januari 31, 2026. Picha na Yanga
Sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly Jumapili iliyopita katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar imeifanya Yanga kuendelea kusalia katika nafasi ya pili ikiwa na pointi tano sawa na FAR Rabat iliyo nafasi ya tatu, Ahly inaongoza ikiwa na pointi nane na JS Kabylie inashika mkia na pointi zake mbili.
Ili Yanga ifuzu robo fainali, inapaswa kuepuka kufungwa na FAR Rabat katika mchezo unaofuata na kisha ipate ushindi dhidi ya JS Kabylie katika mechi ya mwisho nyumbani.
Ama Yanga inapaswa kutopoteza kwa tofauti ya mabao mawili au zaidi dhidi ya FAR Rabat na kuombea timu hiyo ya Morocco ifungwe na Al Ahly katika mechi ya mwisho.
Matokeo mengine yatakayoibeba Yanga ni kupata ushindi dhidi ya FAR Rabat na kisha sare au ushindi dhidi ya JS Kabylie lakini pia ikiifunga FAR Rabat na kisha JS Kabylie iangushe pointi dhidi ya Ahly.
Kiungo wa Azam FC, Yahya Zayd, akijaribu kumtoka mchezaji wa Nairobi United katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyomalizika kwa Azam kushinda bao 1-0. Picha na Azam FC
Azam FC iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Nairobi United katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, juzi Jumapili.
Ushindi huo umeifanya Azam kuwa nafasi ya tatu kwenye kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na pointi sita, Wydad inaongoza ikiwa na pointi tisa sawa na Maniema iliyopo nafasi ya pili na Nairobi United inashika mkia na haina pointi.
Ili Azam FC ifuzu robo fainali inatakiwa ifunge Maniema katika mechi ijayo nyumbani na iombee Maniema ifungwe nyumbani na Nairobi United kisha Azam ishinde mechi ya mwisho ugenini na Wydad.
kinyume na hapo, Ipate ushindi katika mechi mbili zilizobakia dhidi ya Wydad na Maniema. Iwapo Maniema itaifunga Nairobi United basi Azam iifunge Maniema kwa ushindi wa tofauti ya mabao matatu mfano 3-0, 4-1 na kadhalika.
Azam ikifungwa na Wydad basi Maniema ifungwe na Nairobi United. Kisha Azam iifunge Maniema kwa ushindi wa tofauti ya mabao 3matatu.
Beki wa Singida Black Stars (Kulia mwenye nguo nyeupe) akijaribu kumzuia mshambuliaji wa Otoho katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyomalizika kwa Singida BS, kukubali kichapo cha mabao 2-1. Picha na Otoho.
SINGIDA BLACK STARS
Ikiwa ugenini huko Congo, Singida Black Stars jana ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Otoho.
Ili Singida Black Stars ifuzu Robo Fainali inalazimika ishinde mechi zake mbili zilizobakia dhidi ya Belouzdad nyumbani na Stelenbosch ugenini na kuombea Otoho isipate pointi sita kwenye mechi mbili ilizobakiza. Au imalize ikiwa na idadi sawa ya pointi na Otoho na kuhakikisha Stelenbosch haipo juu yake.