Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa mahesabu yoyote ghalati ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu yatakabiliwa na jibu kali. Amesema kuwa Iran imejiandaa kikamilifu kwa makabiliano na kulipiza kisasi.

Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi alitamka hayo jana Jumatatu na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vimejiandaa kutoa jibu kali kwa vitisho vya maadui. “Tunachofikiria ni ushindi tu. Hatuogopi nguvu za kijuu juu za adui, na tuko tayari kikamilifu kwa makabiliano na kumpiga adui kofi la kulipiza kisasi,” amesema Meja Jenerali Mousavi.

Ameongeza kuwa taifa la Iran limesimama kidete kwa muda mrefu dhidi ya kiburi na uchokozi wa Marekani, na kuilazimisha kushindwa kwa mara nyingine tena ikiwa ni pamoja na katika vita vya karibuni, vita  vya pande nyingi na vita vya kigaidi vya hivi karibuni ambavyo vilivuruga hesabu za maadui.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ametamka haya akiashiria machafuko na ghasia za magaidi za karibuni hapa nchini zilizofadhiliwa na Marekani na Israel kwa lengo la kubadili mkondo wa maandamano ya wananchi kuhusu masuala ya kiuchumi na kuwa machafuko. Hata hivyo magaidi hao walikabiliwa na idara ya intelijinsia ya Iran na askari usalama. 

Meja Jenerali Mousavi amesema kuwa kosa dogo la adui litatoa mwanya kwa Iran kuchukua hatua. “Dunia itashuhudia sura tofauti ya Iran yenye nguvu na hakuna Mmarekani atakayekuwa salama, na moto wa kanda hii utaiunguza Marekani na waitifaki wake”, amesisitiza Jenerali Musavi. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *