Bei za mafuta ghafi ya petroli zilipanda Alhamisi duniani kufuatia kurejea kwa mashambulizi ya kijeshi baada ya uchokozi wa Marekani na ukiukaji wake wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Iran. Mvutano huo umeongeza wasiwasi kuhusu usambazaji wa nishati duniani pamoja na kuendelea kwa usumbufu wa usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz.

Hatima za mafuta ghafi ya Brent ziliongezeka kwa dola 1.48, sawa na asilimia 1.6, na kufikia dola 94.58 kwa pipa, huku mafuta ya West Texas Intermediate (WTI) ya Marekani yakiongezeka kwa dola 1.71, au asilimia 1.9, na kufikia dola 91.74 kwa pipa.

Ongezeko hilo lilifuatia taarifa za mashambulizi mengine ya Marekani dhidi ya  Iran na jibu la Tehran kwa kutangaza kuwa Mlango wa Hormuz unafungwa kwa meli zote ziwe za mizigo au mafuta.

Njia hiyo ya baharini ni miongoni mwa njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa nishati, ikipitisha takribani asilimia 20 ya shehena za mafuta na gesi za dunia katika hali za kawaida.

Wachambuzi wanasema kuongezeka huku kwa mvutano kumeimarisha hofu kwamba mtiririko wa nishati kutoka Ghuba ya Uajemi unaweza kuendelea kuwa katika vikwazo vikubwa, jambo linaloendeleza presha ya kupanda kwa bei za mafuta ghafi.

Mchanganyiko wa sintofahamu za kijiografia na kisiasa, misukosuko ya usambazaji, na kupungua kwa akiba umeendelea kuweka bei za mafuta katika viwango vya juu, licha ya jitihada za hivi karibuni za wazalishaji wa OPEC+ kuongeza uzalishaji.

Uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran unatarajiwa kuwa na athari ya haraka kwa bei za mafuta na masoko ya nishati duniani.

Wakati huo huo, serikali ya Ethiopia inatarajia matumizi ya jumla kuongezeka katika mwaka ujao wa fedha hasa kutokana na gharama zinazohusishwa na vita vya Marekani na Isarel dhidi Iran. Akizungumza leo Alhamisi Waziri wa Fedha Ahmed Shide amesema katika hotuba ya bajeti kwamba matumizi ya jumla yanakadiriwa kuongezeka hadi takribani birr trilioni 2.34, sawa na dola bilioni 14.69, katika mwaka wa fedha wa 2026/27 unaoanza mwezi ujao, kutoka birr trilioni 1.92 katika mwaka wa sasa wa fedha.

Amewaambia wabunge kuwa, ongezeko hili kwa kiasi kikubwa limezingatia gharama zinazohusiana na mzozo wa Mashariki ya Kati.

Uchumi mwingi wa mataifa mengi ya Afrika unaendelea kuteseka kutokana na athari za vita haramu vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *