Mchambuzi wa soka na gwiji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, amebadili msimamo wake kuhusu kiungo wa Liverpool, Florian Wirtz, baada ya awali kumkosoa kufuatia mwanzo mgumu wa msimu.

Wirtz alijiunga na Liverpool majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 116 milioni (Sh413 bilioni), lakini alianza taratibu akishindwa kufunga au kutoa pasi ya bao katika Ligi Kuu ya England hadi mwezi Desemba.

Hali hiyo ilimfanya Carragher kueleza wasiwasi wake, akidai nyota wa kigeni waliowahi kuja England walipaswa kung’ara mapema.

Hata hivyo, hali imebadilika. Wirtz sasa amefunga mabao manne katika mechi saba za mwisho za ligi, pamoja na bao alilofunga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Qarabag. Mabadiliko hayo ya kiwango yamemfanya Carragher kubadili kauli.

Kiungo mshambuliaji wa Liverpool, Florian Wirtz, akishangilia bao katika ushindi wa 4-1 iliopata Liverpool dhidi ya Newcastle, Februari Mosi, 2026 katika mechi ya Ligi Kuu England. Picha na Mtandao

Carragher amesema Wirtz ni mchezaji wa kipekee na ana uwezo wa kufikia kiwango cha nyota wa zamani wa Manchester City, Kevin De Bruyne.

“Ligi Kuu imempoteza Kevin De Bruyne, lakini imempata Florian Wirtz. Huyu ni mchezaji maalumu. Ana mvuto kama David Silva, lakini pia ana ubunifu wa aina yake,” amesema Carragher.

Carragher ameongeza kuwa Wirtz sasa anajiamini zaidi, akisema kuna wakati alionekana kama mtoto alipocheza dhidi ya Manchester City ugenini, lakini sasa ana nafasi ya kujibu kejeli hizo atakapokutana nao Anfield.

Washambuliaji wa Liverpool, Hugo Ekitike (Kulia) na Florian Wirtz (Kushoto) wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 4-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle, uliopigwa Februari Mosi, 2026. Picha na Mtandao

Amlinganisha Ekitike na Torres

Mbali na Wirtz, Carragher pia amempongeza mshambuliaji Hugo Ekitike, akidai ni mchezaji bora zaidi kuliko Fernando Torres aliyewahi kung’ara Liverpool kati ya mwaka 2007 na 2011.

Ekitike alijiunga na Liverpool msimu huu kwa Pauni 79 milioni (Sh276 bilioni) kutoka Eintracht Frankfurt na tayari amefunga mabao 15 katika mashindano yote. Alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa 4-1 dhidi ya Newcastle mwishoni mwa wiki, akionyesha ushirikiano mzuri na Wirtz.

Carragher amesema Ekitike ana uwezo mkubwa hata kama hatofikia idadi ya mabao ya Torres.

“Torres alipata mafanikio makubwa kwa sababu ya Steven Gerrard. Ekitike anaweza kucheza bila kumtegemea sana Wirtz, lakini kama ushirikiano wao utaendelea, anaweza kufikia mafanikio makubwa,” amesema Carragher.

Kwa mujibu wa Carragher, kiwango cha wachezaji wapya kinaipa matumaini Liverpool wanapoanza kufikiria maisha mapya, huku kocha Arne Slot akiendelea kujenga kikosi cha ushindani kwa ajili ya siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *