Siku ya Jumanne (Februari 3), msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karoline Leavitt, alithibitisha kwamba mjumbe maalum wa Trump, Steve Witkoff, amekuwa akipanga kukutana na maafisa wa Iran baadaye wiki hii, hiyo ikiwa ni mara ya mwanzo kwa White House kutambuwa uwepo wa mazungumzo hayo.
“Mazungumzo haya bado yanapangwa hadi muda huu. Daima Rais Trump anataka kutumia diplomasia kwanza, lakini hapana shaka kidole kimoja hakivunji chawa. Unahitaji kuwa na mshirika mwenye dhamira ya kufikia diplomasia, na hicho ndicho kitu ambacho mjumbe maalum Witkoff anachokisaka na kukijadili,” alisema Leavitt, ambaye, hata hivyo, aliongeza kuwa bado “rais ana njia nyingi za kuchaguwa mezani pake kuhusiana na Iran.”
Taarifa kutoka vyanzo vyengine ndani ya Tehran na Washington zilisema mazungumzo hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika siku ya Ijumaa, lakini hakuna upande uliothibitisha mahala yatakapofanyika.
Iran, hata hivyo, imeashiria huenda yakafanyika ama nchini Uturuki, Oman au nchi nyengine kwenye ukanda huo, “ambazo zimeonesha hamu ya kuwa wenyeji wa mazungumzo hayo.”
Trump, kwa upande wake, amekataa kuondosha uwezekano wa hatua za kijeshi, na mwenzake wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kwamba mazungumzo hayo yatafanyika endapo tu hayaambatanishwi na kauli za vitisho.
Majeshi ya Marekani, Iran yakwaruzana
Kauli ya Leavitt ilitoka muda mchache baada ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani kutangaza kwamba ndege yake imeidunguwa droni ya Iran iliyokuwa ikiikaribia meli ya kivita ya USS Abraham Lincoln kwenye Bahari ya Arabuni.
Msemaji wa Kamandi hiyo, Kapteni Tim Hawkins, amesema kwamba ndege chapa F-35C kutoka meli hiyo iliiangusha droni ya Iran kama njia ya kujilinda dhidi ya mashambulizi.
Kuangushwa kwa droni hiyo lilikuwa tukio la pili baina ya mahasimu hao kwenye bahari za Mashariki ya Kati hiyo hiyo jana, baada ya jaribio la majeshi ya Iran kuishikilia meli moja inayopeperusha bendera ya Marekani kwenye Mlango Bahari wa Hormuz.
Washington na Tehran zimekubaliana kuzungumza baada ya vitisho vya mara kadhaa vya Trump kuchukuwa hatua za kijeshi, huku nayo Iran ikionya kwamba itajibu mashambulizi hayo kwa kuvilenga vituo vya kijeshi na maslahi ya Marekani kwenye ukanda wote wa Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati.
Marekani ilivilenga vituo vya nyuklia vya Iran mnamo mwezi Juni mwaka jana katika kipindi ambacho Israel ilikuwa ikiendesha vita vyake dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu vilivyodumu kwa siku 12.
Katika siku za karibuni, Pentagon imetuma meli na vifaa kadhaa vya kivita kwenye eneo hilo, tangu maandamano ya kuipinga serikali ya Tehran mwezi uliopita.