
Dar es Salaam. Aliyekuwa mwimbaji wa taarabu, Ally Star, anatarajiwa kuzikwa leo Jumatano Februari 4, 2026 nyumbani kwao Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro.
Ally Star amefariki dunia jana Jumanne Februari 3, 2026 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa TOT, Khadija Kopa ambaye pia ni muimbaji wa taarabu, amesema safari ya kwenda Kilosa itaanza imeanza saa 2 asubuhi na mazishi yatafanyika mara tu baada ya kuwasili.
“Ally Star atazikwa nyumbani kwao Kilosa Kichangani, hivyo safari itaanzia Hospitali ya Muhimbili ambapo waombelezaji wote watakutana hapo kuanzia saa 1 asubuhi, na atazikwa mara tu tutakapofika Kilosa,” amesema Khadija Kopa.
Enzi za uhai wake, Ally Star aliiambia Mwananchi kuwa, mwili wake ulikuwa unapiga shoti kama umeme, hali ambayo ilikuwa ikimpa maumivu makali na kudhoofisha mwili wake.
Katika maisha ya muziki, Ally Star aliimba nyimbo maarufu kama Zumbukuku, Limbukeni, Natanga na Njia, Hauvumi Lakini Umo na nyingine nyingi.
Ally Star aliwahi pia kuzitumikia bendi kama Muungano Cultural Troupe, Orchestra King Kikii Double O na Bima Modern Taarab.