
Watu wasiopungua 15 wamefariki baada ya boti ya doria ya walinzi wa pwani ya Ugiriki kugongana na boti iliyowabeba wahamiaji nje ya pwani ya kisiwa cha Chios Jumanne usiku.
Taarifa ya walinzi wa pwani iliyotolewa Jumatano imesema kwamba hadi sasa, miili 15 imeopolewa yote ikiwa ni ya wahamiaji. Taarifa hiyo imeongeza kuwa wahamiaji 25 walipelekwa katika hospitali ya kisiwa hicho, wakiwemo watoto 11 pamoja na maafisa wawili wa walinzi wa pwani. Wizara ya afya imesema miili 14 iliopolewa baharini, na mwathirika mmoja alifariki baadaye hospitalini.
Walinzi wa pwani waliripoti kwamba makumi ya wahamiaji walikuwa ndani ya boti ya kasi yenye injini iliyo na nguvu iliyokuwa ikisafiri kutoka Uturuki kuelekea Chios. Ilidaiwa kuwa nahodha wa boti hiyo alishindwa kutii amri ya walinzi wa pwani ya kusimama.