Ripoti ya mwaka ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch inatoa taswira ya kutisha, inayopaka rangi ya damu, machozi na ukimya wa dunia. Ripoti hiyo ya dunia ya mwaka 2026, yenye kurasa 529, inaweka wazi ukweli mchungu: raia wa kawaida ndio wamekuwa walengwa wakuu wa vita na siasa kandamizi, hususan katika Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya zaidi ya nchi 100 zilizochunguzwa duniani, Sudan, Sudan Kusini na Ethiopia zimetajwa miongoni mwa maeneo mabaya zaidi kwa raia. Katika nchi hizo, makosa ya kivita, mauaji ya kiholela na mashambulizi dhidi ya wakimbizi yameendelea kufanyika bila wahusika kuwajibishwa ipasavyo.
Ripoti inaeleza kuwa wananchi wasio na hatia mara kwa mara hugeuzwa malengo ya mashambulizi ya kijeshi, huku mifumo ya haki ikishindwa kuwafikisha wahusika mbele ya sheria. Hali hii imechangia kuongezeka kwa mateso ya raia na majanga ya kibinadamu yasiyo na kikomo.
Nchini Sudan, vita kati ya jeshi la serikali na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) vimegeuka kuwa janga kubwa la kibinadamu, likiwaacha mamilioni bila makazi, chakula na huduma za msingi. Ripoti pia inaeleza kuwa vikosi vya serikali navyo vimetuhumiwa kuwalenga raia na miundombinu ya kiraia kama sehemu ya operesheni zao za kijeshi.
Migogoro ya kudumu na aibu ya uwajibikaji
Chacha Nyaigoti Chacha, mchambuzi wa masuala ya kimataifa, anaeleza kuwa mgogoro wa Sudan Kusini umeendelea kuwa doa katika juhudi za bara la Afrika kujipatia amani ya kudumu.
“Sudan Kusini ni donda sugu ambalo limekataa kupona na ni moja wapo ya aibu kubwa kabisa ya uwezo wa Afrika kutafakari na kutafuta utatuzi, tukitarajia kuwa Amerika itatuletea amani.”
Hali ya haki za binadamu nchini Kenya iliendelea kuwa ya kutia wasiwasi katika kipindi cha mwaka uliopita. Ripoti inaonyesha kuwa mamlaka zilikandamiza maandamano ya amani, huku vikosi vya usalama, hasa maafisa waliovalia kiraia, wakituhumiwa kwa utekaji nyara, mateso na kutowesha kwa nguvu waandamanaji na wanaharakati wa mitandaoni.
Katika taifa jirani la Tanzania, hali ya haki za binadamu ilidorora zaidi mwaka 2025, hasa wakati wa uchaguzi uliomrejesha madarakani Rais Samia Suluhu Hassan mwezi Oktoba. Uchaguzi huo ulikumbwa na ukiukaji mkubwa wa haki, ikiwemo matumizi ya nguvu za kuua dhidi ya waandamanaji siku ya uchaguzi.
Ripoti inabainisha kuwa hatua ya kuzimwa kwa intaneti kote nchini ilichangia kuficha ukubwa wa ukiukaji huo, huku mamia ya raia wakiripotiwa kuuawa au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Demokrasia kwenye msukosuko Afrika Mashariki
Allan Ngari, Mkurugenzi wa Ushawishi wa Human Rights Watch barani Afrika, anasema ripoti hiyo inaangazia kwa kina kurudi nyuma kwa demokrasia na athari zake kwa migogoro inayoendelea.
“Ripoti yetu ya leo inazingatia mambo machache ya Afrika: kurudi nyuma kwa demokrasia, athari zake kwa migogoro inayoendelea, na jinsi asasi za kikanda zinavyojibu au kushindwa kujibu wakati raia wanapoathiriwa.”
Hali ya haki za binadamu nchini Uganda nayo imeendelea kuwa kandamizi, huku serikali ikitumia nguvu dhidi ya upinzani wa kisiasa, waandishi wa habari na waandamanaji. Ripoti inaonyesha kuwa uhuru wa kujieleza na kukusanyika umeendelea kudhibitiwa vikali.
Vyombo vya usalama nchini humo vimetuhumiwa kwa kukamata, kupiga na kuwatesa wafuasi wa upinzani na wanahabari, hasa wakati wa kampeni za kisiasa na chaguzi ndogo za ubunge.
Human Rights Watch sasa inatoa wito kwa serikali za kimataifa, taasisi za kikanda na Umoja wa Afrika kuchukua hatua madhubuti za kulinda raia, kusimamia uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha wahusika wa ukiukaji wa haki za binadamu wanawajibishwa kisheria.
