Serikali imetoa wito kwa wadau kutoka sekta ya fedha nchini kuanzisha huduma na bidhaa za kifedha zitakazowezesha ajenda ya nishati safi ya kupikia kusambaa zaidi, hususan kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo katika maeneo ya pembezoni na vijijini pamoja na wabunifu wa teknolojia za matumizi ya nishati hiyo.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba tarehe 4 Februari 2026 wakati akimwakilisha Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi katika uzinduzi wa mradi wa nishati safi ya kupikia katika shule ya sekondari Bunge Wasichana iliyopo mkoani Dodoma.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, matumizi ya nishati hii yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 na kufikia asilimia 23.2 mwaka 2025. Hata hivyo, bado takribani asilimia 77 ya kaya nchini zinatumia nishati isiyo safi ya kupikia, hivyo natoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kusukuma ajenda hii kwa kuwezesha upatikanaji wa nishati mbalimbali safi za kupikia katika maeneo ya pembezoni na yale ya vijijini.” Amesema Mhe. Salome
Aidha, Mhe. Salome amewasisitiza Wasambazaji wa gesi za mitungi kuongeza vituo vya usambazaji na ujazaji wa gesi za mitungi ili kurahisisha upatikanaji wake kwa watumiaji wengi zaidi, pia Wabunifu na vijana walioko vyuoni kufanya tafiti na kubuni nyenzo na teknolojia zitakazowezesha ajenda hii kusambaa na kuwafikia watu wengi.
Kuhusu mradi wa nishati safi ya kupikia aliouzindua Mhe. Salome amesema kuwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za binadamu na kutunza mazingira.
Ameongeza kuwa mfumo huo uliozinduliwa utawezesha chakula kupikwa kwa usafi, kwa haraka, kwa ufanisi, kwa gharama nafuu na bila madhara ya moshi kwa wapishi na wanafunzi huku mazingira yakiendelea kustawi.
Mhe. Salome ameeleza kuwa kuzinduliwa kwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za kitaifa zinazoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034 ambapo mpaka sasa tayari asilimia 23.2 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia.

(Feed generated with FetchRSS)