Onyo hilo lililotolewa leo na Mfumo wa tathimini ya Uhakika wa Chakula IPC, linaonesha kwamba mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan unaendelea kuwa mbaya zaidi, na sasa maeneo mawili zaidi katika jimbo la Darfur Kaskazini ya Um Baru na Kernoi yameingia katika baa la nja kufuatia utapiamlo wa kupindukia au unyavuzi kuvuka wiwango vya kutokuwa na uhakika wa chakula.
Tahadhari hiyo inaonesha kuwa zaidi ya nusu ya watoto katika baadhi ya maeneo Sudan wanakabiliwa na unyavuzi, hali inayohusishwa na mzozo unaoendelea, ufurushwaji mkubwa wa watu, uhaba wa chakula na upatikanaji mdogo wa misaada.
Tahadhari hiyo ya IPC inaonya kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi katika maeneo mengi yasiyofikika, ikitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na kufunguliwa kwa njia salama za misaada ili kuokoa maisha, hasa ya watoto.
Uchambuzi wa hivi karibuni wa IPC, uliochapishwa Novemba 2025, uligundua hali ya njaa kali, ya kiwango cha daraja la 5, katika miji ya El Fasher na Kadugli. Tathmini hiyo ilibaini maeneo 20 yaliyo katika hatari ya baa la njaa huko Darfur na Kordofan.
Wafanyakazi wa afya wanamchunguza mtoto kwa upungufu wa lishe katika kituo cha lishe kinachoungwa mkono na UNICEF huko Tawila, Darfur Kaskazini, Sudan.
Unyafuzi umefikia kiwango cha juu sana
Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kwamba maeneo mawili, Um Baru na Kernoi, yamezidi vizingiti vya kutokuwa na uhakika wa chakula kwa watoto. Katika Um Baru, kiwango cha jumla cha utapiamlo mkali kati ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kilifikia asilimia 52.9, wakati katika eneo la Kernoi ulifikia asilimia 34.
Huku nchini kote, zaidi ya asilimia 60 ya maeneo yaliyotathiminiwa kati ya Januari na Julai 2025 yameripoti kiwango cha hatari.
Mashambulizi dhidi ya mashamba ya kilimo yamesababisha zaidi ya watu milioni 21 kuwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula .
Kuongezeka kwa mapigano kunaendelea kuathiri uzalishaji wa chakula, masoko, na ufikiaji wa huduma za msingi.
Mtoto wa Sudan katika KAMBI ya DALI, TAWILA – Darfur. Familia yake ilikimbia El Fasher, ambapo njaa iliyokuwa ikiendelea ilithibitishwa mnamo Oktoba 2025
Wagonjwa wa unyafuzi watarajiwa kuongezeka
Kufikia mwaka huu 2026, idadi ya wagonjwa wa utapiamlo mkali au unyavuzi inatarajiwa kufikia milioni 4.2, ikilinganishwa na milioni 3.7 waliorekodiwa mwaka uliopita, kwa mujibu wa tahadhari hiyo ya IPC katika muktadha wa ufurushwaji wa watu wa muda mrefu na kuanguka kwa mifumo ya afya, maji, na chakula.
Licha ya mahitaji ya dharura, ufikiaji wa kibinadamu unabaki kuwa mdogo sana kutokana na hali ya usalama, vizuizi, na vikwazo vya kiutawala.
Kuanguka kwa mji wa El Fasher mwezi Oktoba 2025 kulisababisha moja ya ufurushwaji mkubwa zaidi wa watu tangu kuanza kwa mzozo, na zaidi ya watu milioni 1.2 kulazimika kuondoka kutoka eneo hilo kufikia mwisho wa mwaka.
Kordofan, kuongezeka kwa mapigano kunaendelea kuathiri uzalishaji wa chakula, masoko, na ufikiaji wa huduma za msingi.
Ukosefu wa usalama na kuzingirwa kwa miji kama Kadugli na Dilling kunasukuma watu wengi zaidi kufikia viwango vya juu vya njaa.
Athari za mchanganyiko wa mzozo, watu kufurushwa na vizuizi vya ufikiaji zinaharakisha baa la njaa, utapiamlo, kuenea kwa magonjwa, na vifo vinavyoweza kuzuilika, hasa miongoni mwa watoto, wanawake wajawazito, na makundi hatarishi.
Maelfu bado wamenaswa katika miji ya Kordofan, Darfur na El Fasher, ambako vita vinaendelea kupamba moto.
Mapendekezo na hatua za kimataifa
Hatua za kimataifa pia zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa rasilimali. Mpango wa Hatua za Kibinadamu kwa 2026 kwa ajili ya Sudan ulikuwa na ufadhili wa asilimia 5.5 tu mwanzoni mwa Februari. Hali hii inaathiri uwezo wa mashirika kutoa msaada muhimu kabla ya msimu wa mvua.
Tathmini imebaini maeneo 20 yaliyo katika hatari ya njaa huko Darfur na Kordofan.
Inakadiriwa kwamba, kufikia 2026, watu milioni 33.7, takriban sehemu mbili ya tatu ya idadi ya watu wote, watahitaji msaada wa kibinadamu.
Ushirikiano wa IPC, unaojumuisha mashirika 21, ikiwa ni pamoja na mashirika ya kimataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na mashirika yasiyo ya kiserikali, umeonya kuhusu haja ya dharura ya kuchukua hatua mara moja katika mgogoro huu.
Hali ya kufanikisha maboresho na kuzuia vifo zaidi ni kumaliza mapigano na kuruhusu ufikiaji wa kibinadamu bila vizuizi katika maeneo yote.