Watu wanaodaiwa kuwa majambazi wamemjeruhi kwa kumpiga risasi mkazi wa Sogea mjini Tunduma, wilayani Momba, Yengo Mwapina, na kumpora kiasi cha Shilingi milioni 54 akiwa njiani kutokea benki.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, iliyotolewa Februari 4, 2026, tukio hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha lilitokea jana saa 4:00 asubuhi katika eneo la Kisimani, Mtaa wa Unyamwanga, Kata ya Tunduma.

Kamanda Senga amesema Mwapina alivamiwa na watu watatu wasiojulikana na kushambuliwa kabla ya kuporwa fedha hizo alizokuwa ametoka kuchukua katika Benki ya NBC Tunduma.

Ameeleza kuwa kabla ya kupora fedha hizo, watuhumiwa walimfyatulia risasi Mwapina na kumsababishia jeraha la risasi kiunoni upande wa kushoto, kisha kutokomea kusikojulikana wakiwa na fedha hizo.

Kamanda Senga amesema Polisi Mkoa wa Songwe wanaendelea na uchunguzi wa kina pamoja na msako mkali ili kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo na kuwafikisha mahakamani kwa hatua za kisheria.

#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *