Tulidhani sherehe ya kutahiriwa kaka yetu

Catherine ambaye ni Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kiraia la AfyAfrika katika mahojiano na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa anakumbuka siku hiyo akisema, “nilidhani ni sherehe, sikujua kilichokuwa kinakuja”

Yeye anatoka jamii ya wamaasai, ambapo kwa muda mrefu ukeketaji wa wasichana umechukuliwa kama sehemu ya mila na njia ya mpito kuelekea utu uzima. Anakumbuka siku ambayo kaka yake mkubwa alikuwa anaenda kutahiriwa kwenye sherehe kubwa ya kijamii.

Kikundi cha vijana wenye tabasamu wakiwa wamevaa t-shirts za rangi ya manjano zenye nembo za alama za vidole wakipiga picha kwa shauku kwenye hafla ya kampeni ya UNFPA Kenya ya kukomesha ukandamizaji wa uzazi wa kike.

© Afyafrica

Vijana kwenye Afyafrika kampeni ya uhamasishaji kuhusu kutokomeza FGM huko Narok nchini Kenya.

“Siku hiyo, mimi na dada yangu tuliambiwa pia tutashiriki kwenye sherehe. Tulifurahi, hatukujua kinachoendelea,” anasema Catherine.

Usiku wa manane, walichukuliwa kwa siri, wakaogeshwa maji baridi na kupelekwa kwenye chumba ambacho kilikuwa na wanawake watano na zana za ukeketaji. Licha ya hofu na mshtuko, waliambiwa wasilie kwani walikuwa “wanaingia utu uzima”.

Elimu haikutosha kuzuia mila

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba wazazi wa Catherine walikuwa wasomi — baba yake akiwa daktari na mama yake mwalimu. Hata hivyo, hawakuweza kukwepa shinikizo la mila.

“Walitumia ganzi, lakini bado tuliona damu. Dada yangu alizimia. Mimi nililia licha ya kuambiwa nisiwe mwoga,” anakumbuka.

Baada ya tukio hilo, walitengwa kwa mwezi mmoja, hawakuruhusiwa kuzungumza na mtu yeyote wala kuuliza maswali. “Ulikuwa unaambiwa tu: sasa wewe ni mwanamke.”

Madhara ya kimwili na kiakili yaliyoendelea kwa miaka

Madhara ya ukeketaji hayakuisha siku hiyo. Catherine alipokwenda shule ya sekondari nje ya jamii yake, alilazimika kuishi kwa uongo na ukimya.

“Nilikuwa naogopa kuulizwa kama nimekeketwa. Kulikuwa na dhihaka kwamba wanawake waliokeketwa hawana hisia. Nilijisitiri kimya kimya,” anasema.

Dada yake alijifungia zaidi, akawa mtu wa kimya sana. Catherine naye alianza kujitenga, akijistigmatisha na kuchagua kwa uangalifu nani wa kuzungumza naye.

Mtaalamu wa matibabu katika kanzu nyeupe akizungumza katika tukio huko Narok, Kenya, akiendeleza mradi wa Linda Msichana, ambao unakusudia kukomesha ukataji wa viungo vya uzazi wa kike (FGM) kwa msaada wa UNFPA na AfyAfrika.

© Afyafrika

Mtaalamu wa matibabu akiwasilisha mradi wa Linda Msichana wa kukomesha FGM huko Narok, Kenya.

Safari ya uponyaji na kuvunja ukimya

Baada ya miaka mingi ya maumivu ya ndani, Catherine alipata msaada kupitia shirika la kiraia la The Girl Generation, lililowaunganisha manusura wa ukeketaji kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya.

“Kupitia vikao vya msaada wa kisaikolojia, niligundua sikuwa peke yangu. Tulirudi kwenye majeraha ya utotoni na kuanza safari ya kupona,” anaeleza.

Ilimchukua takribani miaka mitano kujikubali, kujisamehe, na hata kuwasamehe wazazi wake. Hatimaye, baada ya miaka 23 ya ukimya, aliamua kusimulia hadithi yake hadharani.

AfyAfrika: Kutumia hadithi binafsi kuleta mabadiliko

Mwaka 2007, Catherine alianzisha AfyAfrika, shirika linaloongozwa na vijana kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu madhara ya ukeketaji na kuboresha afya na ustawi wa vijana waliotengwa.

“Wengi hawajui kinachotokea wakati wa ukeketaji, hasa wanaume. Nilitaka jamii ijue ukweli,” anasema.

Kupenya katika jamii ambako wanawake hawapewi nafasi ya kuzungumza mbele ya wanaume haikuwa rahisi, lakini Catherine na wenzake waliendelea kusukuma ajenda ya mabadiliko.

Wito wa msaada kwa manusura

Catherine anasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya msaada kwa manusura wa ukeketaji, hasa huduma za kisaikolojia.

“Tunahitaji wanasaikolojia zaidi, mifumo ya msaada, na jamii zinazokubali manusura bila hukumu,” anasema.

Watoto wanashiriki katika mbio za mbio wakati wa tukio la kampeni ya uhamasishaji wa UNFPA Kenya FGM huko Narok, kuonyesha ushiriki wa jamii na ushiriki wa vijana.

© Afyafrika

Michezo ya watoto katika kampeni ya uhamasishaji kuhusu FGM huko Narok Kenya inayoongozwa na shirika la Afyafrika.

Mustakabali wa kutokomeza ukeketaji

Kuhusu hatma ya ukeketaji nchini Kenya, Catherine ana matumaini ya akisema “tunaona juhudi za sekta mbalimbali. Huenda hatujafika asilimia 100, lakini tunaelekea mahali pazuri,” anahitimisha.

Kuhusu AfyAfrika
AfyAfrika ni shirika linaloongozwa na vijana, lililoanzishwa mwaka 2007 mjini Narok, Kenya. Linalenga kuboresha afya, elimu, na kujitegemea kwa vijana waliotengwa kupitia uhamasishaji, mafunzo, utetezi, utafiti na ushiriki wa kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *