Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ameshauri kampeni ya upandaji miti mkoani Dodoma iyahusishe kwa kiwango kikubwa makundi ya vijana ili kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa, inakua na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

Pinda amesema vijana ni kundi kubwa nchini, hivyo kwa wingi wao wana uwezo wa kufanikisha kampeni ya kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kijani kwa kupanda na kutunza miti kwa kushirikiana na serikali za mitaa.

Ametoa ushauri huo leo Ijumaa, Februari 6, 2026 jijini Dodoma wakati akiongoza shughuli ya upandaji miti katika kilima kilichopo eneo la Njedengwa, akishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti ununuzi wa umma (PPRA) akizungumza na waandishi wa habari kwenye shughuli ya kupanda miti leo, Februari 6, 2026 Jijini Dodoma

Amesema serikali, kwa kushirikiana na viongozi wa mashina na matawi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), inaweza kuongoza shughuli za upandaji na utunzaji wa miti kwa kipindi cha mwaka mzima, jambo litakalosaidia kuonekana kwa matokeo chanya.

“Mnaweza kufanya mzunguko wa kata kwa kata au mtaa kwa mtaa ambapo vijana watakuwa wanapanda na kuitunza miti. Kuhusu suala la maji si tatizo, kwani hata maji yaliyooshewa vyombo yanaweza kutumika kumwagilia miti na ikaendelea kukua,” amesema Pinda.

Ameongeza kuwa wananchi wengi hawaielewi kikamilifu kampeni ya upandaji miti kwa sababu huona bado kuna miti mingi, hivyo kujiuliza sababu ya kupanda mingine.

Hata hivyo, amesema hawazingatii kasi kubwa ya ukataji miti inayoendelea pamoja na kushindwa kutekelezwa kwa kauli mbiu ya ‘kata mti, panda mti’.

“Hakuna mtu anayekata mti anayefikiria kupanda mti mwingine, ndiyo maana kampeni hii inapaswa kupewa uzito mkubwa,” amesema.

Pinda amesisitiza kuwa shughuli za upandaji miti nchini hazipaswi kufanyika kwa nyakati maalumu pekee, ikiwemo maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Rais, bali ziwe endelevu kwa lengo la kutunza mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema kampeni ya kuujani­sha mkoa huo ni endelevu tangu ilipozinduliwa mwaka 2017 na Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa Makamu wa Rais. Amesema kila mwaka mkoa huo hujiwekea lengo la kupanda miti milioni 1.5.

Amesema kupitia kampeni hiyo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongeza bajeti ya utunzaji mazingira kutoka Sh700 milioni hadi Sh3.5 bilioni ili kuhakikisha shughuli za upandaji na utunzaji wa miti zinafanikiwa.

“Ili kuhakikisha miti inayopandwa haifi, tumekuja na kampeni ya kupanda miti ya matunda ambayo pamoja na kutoa kivuli, pia ina manufaa ya kiuchumi kwa kuzaa matunda na kuongeza kipato cha familia,” amesema Senyamule.

Baadhi wa wanafunzi na wadau wa mazingira walioshiriki shughuli ya kupanda miti leo eneo la Njedengwa Jijini Dodoma.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, amesema ili kuhakikisha miti 1,000 iliyopandwa leo haifi, mamlaka hiyo itaviwezesha vikundi vitatu kupitia mfumo wa ununuzi wa umma kuitunza miti hiyo, akisisitiza kuwa hakuna mti hata mmoja utakao kufa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *