
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa mazungumzo yaliyopangwa kufanyika na Marekani yatalenga suala la kutotekelezwa kwa kifungu cha kwanza cha Waraka wa Makubaliano (MoU) uliosainiwa hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, ameyasema hayo Jumapili kabla ya mazungumzo kati ya wajumbe wa Iran na Marekani katika eneo la Burgenstock, Uswisi.
Amesema: “Kuanza kwa mazungumzo ya kufikia makubaliano ya mwisho kunategemea masharti matano mahsusi, ikiwemo kifungu cha kwanza cha MoU, ambacho kinahusu kusitishwa kwa uhasama katika nyanja zote, ikiwemo Lebanon.”
Ameongeza kuwa: “Tunafahamu kwamba kifungu hiki hakijatekelezwa na kwamba Marekani ama haijaweza au haikutaka kukitekeleza. Utawala wa Kizayuni unaendelea kukiuka ahadi zake. Hili ndilo suala kuu katika mazungumzo ya leo.”
Msemaji huyo pia amesisitiza kuwa mkutano huo uliopangwa unaonyesha umakini wa Iran katika kufuatilia utekelezaji wa ahadi za upande mwingine.
Ameongeza: “Hatukuwa na nia ya kusaini waraka huku tukitarajia utekelezwe moja kwa moja na upande mwingine; hatusahau kamwe uzoefu wa hapo awali.”
Jumatano, marais wa Iran Masoud Pezeshkian na Donald Trump wa Marekani, walisaini kwa njia ya mtandao Waraka huo wa Makubaliano, unaolenga kukomesha kabisa vita haramu vya uchokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Makubaliano hayo yenye vipengele 14 yanajumuisha ahadi ya pande zote mbili kufanya mazungumzo zaidi katika kipindi cha siku 60 zijazo kwa lengo la kufikia makubaliano ya mwisho.
Waraka huo unatoa wito wa kusitishwa kwa kudumu kwa uhasama katika nyanja zote, ikiwemo Lebanon; kuondolewa kwa hatua kwa hatua kwa vikwazo vya Marekani; kuondolewa kwa mzingiro wa majini dhidi ya Iran ndani ya siku 30; pamoja na kurejeshwa kwa shughuli za kibiashara kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Jumamosi, Kamandi Kuu ya Kijeshi ya Iran ilitangaza rasmi kufungwa kwa Lango-Bahari wa Hormuz kwa usafiri wote wa majini, ikitaja ukiukaji wa makubaliano ya Tehran na Washington uliofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni.