Mkoa wa Lindi unatarajia kuanza kambi rasmi ya matibabu ya upasuaji wa mabusha kuanzia Februari 9 hadi 25, 2026, ambapo zaidi ya wananchi 500 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji huo bila malipo.
Kambi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi na kurejesha furaha kwa waathirika wa tatizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amesema kambi hiyo imefadhiliwa na Serikali na itahusisha utoaji wa huduma zote muhimu bila gharama yoyote kwa wananchi watakaonufaika. Amesema huduma hizo ni pamoja na upasuaji, chakula na vinywaji kwa wagonjwa wakati wote wa kusubiri na kupatiwa huduma.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuwaondolea wananchi mzigo wa gharama za matibabu pamoja na matumizi mengine yanayotokana na kusubiri huduma za afya, hasa kwa wananchi wa kipato cha chini.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewahamasisha wananchi wenye tatizo la mabusha kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na kambi hiyo, akisisitiza kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi na usalama.
Mganga mkuu wa mkoa wa Lindi Dk. KHery Kagya amewaalika wananchi kujitokeza Kwa wingi kwani hospital imejikita kuhakikisha inawahudumia wananchi Kwa weledi na kuzingatia misingi ya utoaji huduma za kiafya.
(Feed generated with FetchRSS)