Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kuthibitisha uimara wake kama mhimili wa amani, mshikamano na maendeleo ya Taifa, huku kikitimiza miaka 49 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, kikiwa kimebeba mafanikio makubwa yanayoonekana katika nyanja zote za maisha ya Watanzania.

Akihitimisha maadhimisho ya Miaka 49 ya CCM ngazi ya Mkoa wa Morogoro yaliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Joseph Masunga, amesema Serikali inayoongozwa na CCM imejipambanua kwa kusimamia kwa vitendo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanamgusa kila mwananchi bila kubagua huku akisisitiza viongozi wa Chama hicho kutenga muda wa kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi ipasavyo.

Mhandisi Masunga amesisitiza kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo, “Tumechagua umoja na amani kwa maendeleo ya Taifa letu,” si maneno matupu bali ni falsafa iliyoijenga CCM na Taifa kwa ujumla, akiwataka viongozi wa chama na Serikali kuendelea kuwa karibu na wananchi kwa kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

“CCM imeendelea kuwa nguzo ya amani na umoja wa Watanzania, jambo lililowezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa za maendeleo katika mazingira ya utulivu na mshikamano,” amesema Masunga.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Nuru Ngereja, amesema Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kielelezo cha uongozi bora unaojali maendeleo ya watu, akieleza kuwa mafanikio yanayoonekana katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, miundombinu, maji na nishati ni ushahidi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo.

Akitoa salamu za Mkoa wa Morogoro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Adam Kighoma Malima, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dustan Kyoba, amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu miradi yote ya maendeleo kwa kuzingatia misingi ya uaminifu, uwajibikaji, uadilifu na weledi, ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na kuleta tija kwa wananchi.

#KilichoBoraKabisa

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *