Tabora. Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Mohamedi Said Dimwa, amewasilisha salamu za rambirambi kwa familia za aliyekuwa mjumbe mstaafu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na mmiliki wa Kampuni ya Usafirishaji ya NBS, Nassor Hamdan, pamoja na familia ya aliyekuwa Mbunge mstaafu wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora, Munde Tambwe, waliofariki dunia.
Munde Tambwe alifariki dunia usiku wa kuamkia Februari 3, 2026 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuzikwa Februari 4, katika Makaburi ya Kidongo Chekundu kata ya Ngambo, Tabora.
Nassor Hamdan ambaye ni mmiliki wa mabasi ya NBS Tabora, alifariki dunia Februari 2, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza leo Ijumaa Februari 6, 2026 kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, Dimwa amesema salamu hizo ni sehemu ya faraja kwa familia zilizofiwa, sambamba na kutambua mchango mkubwa wa marehemu hao katika kulitumikia taifa na chama kwa uadilifu.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha akikabidhi rambi rambi kwa niaba ya viongozi wa kitaifa kwa mtoto wa marehemu Nassor Hamdan, Zuhra Nassor.
Amesema Rais Mwinyi ametoa pole kwa familia hizo pamoja na wakazi wa Mkoa wa Tabora kwa kuwapoteza viongozi waliogusa maisha ya jamii, hususan katika nyanja za uongozi na uchumi.
“Tuko pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu. Msione kama mmekuwa peke yenu, tutaendelea kushirikiana kama ilivyokuwa awali. Tuendelee kuwa watulivu huku tukimuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu,” amesema Dimwa.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Bara, Mhandisi Nassir Juma, amesema marehemu Nassor alikuwa siyo tu kiongozi, bali mshauri muhimu katika masuala ya maendeleo na ujenzi wa chama.
“Tumempoteza mtu mwaminifu na mwenye mchango mkubwa kwa chama na taifa. Kupitia NBS, aliweza kugusa maisha ya wananchi wengi,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha akikabidhi rambirambi kwa niaba ya viongozi wa kitaifa kwa mtoto wa marehemu Munde Tambwe, Almas Iteba.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, ameambatana na viongozi wa kitaifa kuwasilisha salamu za rambirambi kwa familia hizo mbili, akisema amewakilisha viongozi wa kitaifa kama sehemu ya faraja kwa wafiwa.
“Nimeletwa hapa kuwasilisha pole kutoka kwa viongozi wa juu, wakisema wako pamoja nasi katika kipindi hiki cha majonzi,” amesema Chacha.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya marehemu Nassor, mtoto wake wa kwanza, Mohamedi Hamdani, ameshukuru viongozi na jamii kwa kuwa karibu nao tangu mwanzo wa msiba.
Naye Zuhra Nassor amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutenga muda wa kuwafariji, akimuomba aendelee kuwa karibu nao.
“Msituache, kwa sababu kipindi hiki ndicho kigumu zaidi kwetu, lakini tunamshukuru Mungu kwa kila jambo,” amesema.
Kwa familia ya marehemu Munde Tambwe, mtoto wake mkubwa, Almasi Iteba, ametoa shukrani kwa rambirambi zilizotolewa na kuomba wananchi wa Tabora waendelee kuwapa faraja.
“Faraja ya wananchi ndiyo nguzo pekee iliyobaki kwetu kama familia,” amesema.