
Dar es Salaam. Kama umeamua kishi kikamaria, basi tandika mikeka sana. Mpaka Gabachori akusanye virago vyake na kurudi Bombei. ‘Steki’ mzigo siyo kizushi na ‘odsi’ mlima, pigo moja uwe bilionea wa ghafla bin vuu.
Kuweka mkeka wa pesa za bia mbili ni undezi. ‘Teki iti o’ livu iti’, tunataka kulala njaa na kuamka mamilionea. Ndoto za utajiri wa kilimo na ufugaji zilitoweka na virusi vya korona. Mchongo ni mikeka mwanzo mwenga.
Ukiwa mkamaria usilale bila simu kuwa na mkeka wowote. Tandika mkeka wa leo leo na treni la wiki. Chungulia kila wakati ili mabwege kama Pafos ama Slavia Prague, wakichana ‘ribeti’ fasta. Masela utajiri ndo pepo ya duniani.
Wananagu wote kitaa tunataka ‘laifu eksipensivu, tuishi kituristi’. Tutoke magetoni kwenye nondo, vyuma na mabati. Tukaishi kishua katika majengo ya vioo, badala ya ndoto za alinacha tunataka tuone ‘fyucha’ kupitia katika dirisha.
Kwa dada zetu mnaosaka ‘laifu la kituristi’ kwa ujasiriamwili. Tokeni vyumbani humo, acheni kujazana magetoni kipimbi. Jiwekeni safi kisha jichanganyeni maeneo safi ya ‘kituristi’. Shitukeni dunia ya sasa inataka kutega pesa na siyo kusaka.
Acheneni na laifu la ‘kigademiti’ kujianika maeneo ya kinyonge. Mtateswa na kausha damu hadi lini? Mama zenu wale ‘malijendari’ walienda ‘Q Bar, Jolly Club, katika ‘kasino’. Mitego kwa wazungu tu. Na ‘Slogani’ yao waliyoitumia ni ‘No Mane No Hane”.
Wakapata vibabu vya kizungu na kusepa Ulaya. Waliobaki Bongo walipewa maisha kwa kuachiwa mijengo na mbegu, watoto flan chotara. Acheni kudili na walevi waswahili wanahonga matusi badala ya pesa. Kumbukeni pesa mbele kama tai dyadyaa.
Kila mtu apambanie kombe lake, tuache kupangiana michongo ya kufanya. ‘Teki iti o’ livu iti’ hapa ni ‘kumeki moo mane’ siyo ‘kulosti’ na kuwa mjane wa pesa. Jambo lolote ufanyalo hakikisha linanata na “biti’ ya utajiri wa pesa tu.
Na zile pigo za masela kukataa mimba mwisho 2025. Kwa 2026 na kuendelea beba majukumu ya ubaba hata kama wamekujazia tambara tupu. Hivi mnapata wapi ‘pawa’ ya kukataa mimba kizazi cha wanzuki nyie? Hamuogopi aiseee?
Kuna laana nyingi, lakini kukataa damu yako ni laana ‘gredi wani’. Na laana hii inasambaa na kudili na wewe kama kansa ya damu. ‘Blaza’ usikatae, kama wahuni wa kike wamekupakazia, beba kalee mtoto. Damu siyo haramu wala damu siyo sanamu.
Hakuna watu wanatusua ‘kilaifu’ kama waliopakaziwa mimba. Kila tajiri duniani ana watoto kadhaa ambao siyo damu yake. Ambao wapo ndani ya ndoa. Kimsingi siri ya utajiri mkubwa, nawapa leo, ni kulea mimba isiyokuhusu. Beba jukumu.
Tafuta hata mababu zako, ambao walikuwa na maisha flan poa poa. Wengi walilea watoto wasiokuwa damu yao. Jaribu kumchunguza baba au mamaako, kama familia yake ya kishua, huenda yeye siyo damu ya babaake. Familia nyingi za kishua ziko hivyo.
So! Tafuta mtu yeyote mtaani au unayemfahamu popote. Kama dingi kafanana sana na watoto, angalia ‘laifu’ yake. Utakuta ni ya kawaida sana tena anategemea mshahara tu. Sasa tafuta dingi asiendana sura na watoto wake. Lazima awe na pesa tele.
Usiwe mbishi pimbi wewe. Yule tajiri nanii anafanana na watoto wote? Na yule nanii watoto wake wote anafanana nao? Kaangalie hata ‘komenti’ za waja kule mjini insta. Huoni wanavyoponda juu ya damu yake? Vipi ana mkwanja ama njaa njaa kama wewe?
Shituka! Sasa endelea kukataa damu mpuuzi wa mwisho wewe. Utaendelea na maisha ya kuunga unga mpaka unadedi kama paka. Achia moyo, peleka mkwanja kwa mtoto awe na maisha amazing ujipatie baraka. Hata kama sura na kiganja siyo chako komaa.
Kila mchongo unatoboa kirahisi tu kama ukizingatia kanuni. ‘Laifu’ lina kanuni zake, ukizifuata halina ujanja wa kukuacha. Weka pesa nyingi chimbo kisha tumia kiasi, ongeza kasi ya kusaka, na kubali udhaifu wako. Hapo utakuwa sawa kwa kila kitu.
Mfano mimi udhaifu wangu upo kwa totozi nyembamba. Mwaka 1998 Nyerere akiwa hai mzima wa afya. Niliuza kiunga chetu cha minazi kule Ikwiriri kwa sababu ya Benadeta. Kibenadeta kilikuwa chembamba kama magodoro ya hosteli vyuoni.
Baadaye ‘akaolewaga’ na mzungu kutoka nchi za ‘Skandinavia’ huko.
Mtoto alijua kuninyoosha. Halafu hatumii nguve. Mimi ndo nilikuwa na upungufu wa kinga za kujizua kutoa nilichonacho. Akijinunisha tu baaaasi, nitaisaka pesa popote ilipo hadi ipatikane.
Sijilaumu licha ya kufarakana na familia wakati kwa sababu yake. Kwani alinifundisha kusaka pesa zaidi zaisi. Kwani aliponiacha tu, nikaongeza bidii ya kusaka pesa ili kuilipa familia na nilifanikiwa kwa kiasi kikubwa hata kupewa msameha.
Ukipoteza pesa ama mali, acha kujitia unyonge. Amka pangusa makalio yake nenda kazisake tena na tena. Pesa ni ‘malaya’ sana kuliko malaya ydyote katika uso wa dunia hii. Pesa haikatai mtu, haichagui rangi, kabila, asili wala dini. Inaenda kwa yeyote.
Kila mtu awe ‘dem’ au ‘blaza’ pesa inakukubali ukiisaka kweli kweli. Pesa inaenda kwa yeyote awaye. ‘Imejini’ kajitu kafupi vile kama Zakayo kalikuwa kanamiliki utajiri mkubwa enzi za Mfalme Herode na Pilato. Yesu alikuta kamilionea tayari hapa duniani miaka elfu mbili iliyopita.
Kwanini hawakupewa utajiri wale mafarisayo na maafande ambao ni warefu waliomsulubu Yesu? Ila akapewa Zakayo ambaye mfupi kiasi cha kupanda juu ya mti ili amuone Yesu.Lakini tajiri kuliko makutano wote waliokusanyika pale kusikiliza neno.
Ili ujue alikuwa na mkwanja kiasi gani. Aliambiwa ili apige misele na Yesu, akauze mali zake zote na pesa kugawa kwa masikini. Kwa dunia ya leo Zakayo ni kama GSM, Moo, Bakhressa au Shekhie Mansoor. Zakayo alikuwa ‘don’ kweli kweli usipime.
So! Wanangu mkwanja hauna ubaguzi. Tuzisake kwa nguvu na maarifa mengi ili tuishi ‘kituristi, laifu eksipensivu, teki iti oo livu iti’, gademiti’. Masela chomokeni mageto twende tukazisake pesa zipo kwa ajili yetu. Hatuna budi kuzitafuta.
Hata kama ni marioo kwa bibi wa kizungu, ongeza juhudi, bidii na maarifa mengi kwenye eneo lako la kazi mtambuka. Usishushe kile kiwango chako ukatemwa dirisha dogo la usajili. Kaza mwanangu ujihakikishie namba ya kudumu hapo. Kulelewa pia kazi.