Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amewataka wawekezaji wote katika sekta ya madini nchini kuharakisha utekelezaji wa miradi yao ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa, kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Faru Graphite Corporation katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam.
Kampuni hiyo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa madini ya kinywe katika Wilaya ya Mahenge, Mkoa wa Morogoro.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mavunde amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyowezesha kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya madini.
Amebainisha kuwa juhudi hizo zimeongeza imani kwa wawekezaji na kusaidia kuibua miradi mikubwa inayotarajiwa kuleta manufaa ya kiuchumi kwa taifa.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akisalimiana na viongozi wa Kampuni ya Faru Graphite Corporation katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa uwekezaji zimechangia kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Hivyo, ni wajibu wa wawekezaji kuhakikisha wanatekeleza miradi yao kwa wakati ili wananchi na taifa kwa ujumla wanufaike na uwekezaji huo.
“Ni wakati muafaka sasa kwa wawekezaji wote ambao miradi yao bado haijaanza utekelezaji kuunga mkono juhudi za Serikali kwa vitendo kwa kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo. Miradi ya madini ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuongeza mapato ya Serikali na kufungua fursa za ajira kwa wananchi,” amesema Mavunde.
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye dhamira ya dhati ya kuendeleza miradi yao, huku akieleza kuwa matarajio ya Serikali ni kuona miradi iliyopata vibali na kukamilisha hatua muhimu za maandalizi ikianza utekelezaji kwa wakati uliopangwa.
Akizungumzia mradi wa Faru Graphite, Mavunde ameutaka uongozi wa kampuni hiyo kuharakisha hatua za kuanza utekelezaji wa mradi huo pamoja na kuhakikisha malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha eneo la mradi yanakamilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa Mkoa wa Morogoro na taifa kwa ujumla kutokana na uwezo wake wa kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kuongeza shughuli za biashara na kuchangia mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akisalimiana na viongozi wa Kampuni ya Faru Graphite Corporation katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mradi huo wa uchimbaji wa madini ya kinywe unatarajiwa kudumu kwa takribani miaka 26, jambo linaloufanya kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya madini yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo la Mahenge na maeneo jirani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Black Rock Limited, John De Vries, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa katika maandalizi ya mradi huo.
Amesema kampuni hiyo imeendelea kufanya maandalizi muhimu kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa mradi na kwamba changamoto kubwa iliyokuwapo katika kipindi cha hivi karibuni ilikuwa msimu wa mvua ulioathiri baadhi ya shughuli za awali za ujenzi.
De Vries amesema Faru Graphite ipo tayari kuendelea na kazi za awali za ujenzi mara baada ya kumalizika kwa msimu wa mvua na kwamba kampuni hiyo inaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kuhakikisha mradi huo unaanza kwa mafanikio.
Mradi wa Madini ya Kinywe wa Mahenge unatajwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa unaotarajiwa kuimarisha shughuli za uchimbaji madini nchini, kuongeza ajira kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na taifa kwa ujumla.