
Stuart Casey Maslen, mkuu wa Akademia ya Geneva ya Sheria za Kimataifa za Kibinadamu na Haki za Binadamu amesema, tangu Oktoba 2023 hadi sasa, idadi ya watu huko Ghaza imepungua kwa zaidi ya 10%, hali inayoashiria kutokea vifo takribani laki mbili.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu ripoti ya akademia hiyo yenye anuani ya ‘War Watch’, ambayo inazungumzia hali ya Ghaza na migogoro mingine 23 ya utumiaji silaha katika miezi 18 iliyopita, Maslen ameelezea hali ya Ghaza kama “ya kushangaza”.
Huku akibainisha wasiwasi maalumu alionao kuhusu wale waliojeruhiwa ambao wanahitaji kuhamishwa hadi maeneo salama kwa ajili ya kupatiwa matibabu yanayostahiki, Maslen amesema: “watu wanaendelea kufa huko Ghaza.”
Mkuu huyo wa Akademia ya Geneva ya Sheria za Kimataifa za Kibinadamu na Haki za Binadamu ameeleza kwamba inakubaliwa na wote kuwa raia Wapalestina wasiopungua 70,000 wameuawa huko Ghaza tangu Oktoba 2023 hadi sasa na akasisitiza kwa kusema: “hatuamini kama hiyo ndiyo idadi kamili. Hiyo ni idadi ya miili ambayo imepatikana. Kutakuwa na miili zaidi chini ya vifusi. Itachukua muda kabla ya idadi kamili kujulikana. Ripoti ya Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina imeeleza kwamba punguo la idadi ya watu wa Ghaza ni zaidi ya 10%”.
Kuhusiana na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, Maslen amesema: “sidhani kama mauaji ya kimbari huko Ghaza yalianza Oktoba 7, 2023, na ikiwa tunazungumzia tafsiri ya kisheria, basi ni hapana”, na akaongeza kuwa Tume Huru ya Uchunguzi ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa, bila kutaja tarehe, ilisema wazi kwamba mauaji ya kimbari yalifanyika Ghaza.
Aidha, msomi huyo wa masuala ya sheria amesema, dunia bado haijaona upigaji hatua katika ushughulikiaji wa hati za kukamatwa zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). “Badala yake, tumeona vikwazo vikiwekwa dhidi ya majaji waliotoa hati hizo,” ameeleza Maslen.
Amesisitiza kuwa, wanataka kuona haki inatendekea kwa wale wote waliouawa kinyume cha sheria, na kuongeza kuwa, ana uhakika watu wa Ghaza, nao pia wanataka jambo hilohilo…/