Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amezipongeza Pakistan na Qatar kwa juhudi zao alizozitaja kuwa za “kutochoka” katika upatanishi, akisema kuwa hatua kubwa zimefikiwa kuelekea kumaliza vita dhidi ya Iran, lakini akasisitiza kuwa “kipimo halisi” kitakuwa utekelezaji wenye mafanikio wa usitishaji vita nchini Lebanon.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X mapema Jumatatu, Araqchi amesema: “Juhudi, zinazotekelezwa bila kuchoka, za upatanishi za Pakistan na Qatar zimeleta maendeleo makubwa katika kumaliza Vita vya Lebanon. Mauzo ya mafuta na bidhaa za petrokemikali yameondolewa vikwazo, mzingiro umeondolewa, baadhi ya mali zilizokuwa zimezuiwa zimeachiwa, na mpango mkubwa wa ujenzi upya na maendeleo kwa Iran umeanzishwa. Kipimo cha kwanza halisi ni kitengo cha uratibu wa kuzuia migongano nchini Lebanon.”

Kauli za Waziri huyo zilikuja wakati duru ya kwanza ya mazungumzo ya ngazi ya juu ya kiufundi kati ya Iran na Marekani ilipohitimishwa nchini Uswisi. Maafisa wa Iran walithibitisha kuwa mikutano ya pande nne ilisimamishwa baada ya Washington kutoa matamshi ya vitisho, ingawa kazi za kiufundi zitaendelea.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, ambaye alikuwa ameandamana na ujumbe wa Iran ulioongozwa na Spika wa Bunge, Mohammad Baqer Qalibaf, aliwaambia waandishi wa habari mapema Jumatatu kuwa mazungumzo ya Uswisi yalilenga kufuatilia utekelezaji wa ahadi za Marekani chini ya Hati ya Makubaliano (MoU) iliyotiwa saini baina ya nchi mbili Juni 18.

Ameongeza kuwa: “Tumekuwa na siku ndefu sana. Mikutano ilianza Jumapili asubuhi. Wakati wa kikao cha pande nne, matamshi ya vitisho kutoka Marekani yalichapishwa, jambo lililoifanya Iran kutangaza kwamba haitaendelea na mkutano huo chini ya mazingira hayo.” Alikuwa akiashiria vitisho dhidi ya Iran vilivyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumapili.

Baghaei amethibitisha kuwa utekelezaji wa MoU unahitaji kukomeshwa kwa vita “katika medani zote,” bila jambo hilo kutekelezwa, “haiwezekani kuingia katika hatua ya mazungumzo ya makubaliano ya mwisho.”

Amesema pia kuwa maendeleo yamepatikana katika majadiliano kuhusu utoaji wa vibali vinavyohitajika kwa mauzo ya mafuta ya Iran pamoja na kuachiliwa kwa mali zake zilizokuwa zimezuiwa.

Aidha, amethibitisha kuwa utaratibu wa kuhakikisha meli zinapita kwa usalama katika Lango Bahari la Hormuz unaandaliwa.

Qatar na Pakistan zimetoa taarifa ya pamoja zikithibitisha kuwa kikao cha kwanza cha mazungumzo ya ngazi ya juu chini ya Mapatano ya Islamabad kimehitimishwa katika mapumziko ya Bürgenstock nchini Uswisi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pande husika zimekubaliana kuunda Kamati ya Ngazi ya Juu kwa ajili ya kusimamia mwelekeo wa kisiasa wa mchakato huo, huku wajadiliani wakuu wakitoa taarifa za mara kwa mara na kuongoza vikundi kazi vinavyoshughulikia masuala ya nyuklia, vikwazo, pamoja na mfumo wa ufuatiliaji na utatuzi wa migogoro.

Kamati hiyo imekubaliana kuhusu ramani ya utekelezaji inayolenga kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60.

Wapatanishi hao pia wametangaza kuanzishwa kwa njia maalumu ya mawasiliano ili kuzuia matukio yasiyotarajiwa na kuhakikisha meli za kibiashara zinapita salama katika Lango Bahari la Hormuz, pamoja na kuundwa kwa kitengo cha uratibu wa kuzuia migongano kinachohusisha Lebanon ili kuhakikisha kusitishwa kwa operesheni za kijeshi nchini humo kunazingatiwa.

Mazungumzo ya Uswisi ndiyo yalikuwa mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu chini ya Hati ya Makubaliano ya Islamabad yenye vipengele 14, iliyotiwa saini Juni 18 na marais wa Iran na Marekani baada ya miezi kadhaa ya diplomasia iliyopatanishwa na Pakistan.

MoU hiyo inazifunga pande zote mbili kuhitimisha mara moja na kwa kudumu operesheni za kijeshi katika “medani zote”, ikiwemo Lebanon.

Pia inaelekeza kuondolewa kwa mzingiro wa majini wa Marekani ndani ya siku 30, kuachiliwa kwa mabilioni ya dola za mali za Iran zilizokuwa zimezuiwa, pamoja na kuanzishwa kwa mfuko wa dola bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi upya wa Iran.

Hata hivyo, utekelezaji wa makubaliano hayo umekumbwa na changamoto. Licha ya ahadi ya usitishaji vita, vikosi vya Israel vimeendelea kufanya mashambulizi kusini mwa Lebanon, ikiwemo mashambulizi mabaya katika vitongoji vya kusini mwa Beirut yaliyosababisha vifo vya raia kadhaa.

Iran ilijibu Jumamosi kwa kutangaza kuwa imeufunga tena Lango-Bahari la Hormuz, ikiishutumu Marekani kwa kushindwa kutimiza ahadi yake ya kusitisha mapigano nchini Lebanon.

Wakati mazungumzo ya Uswisi yakianza Jumapili, Trump alitoa mfululizo wa vitisho kupitia mtandao wake wa kijamii na katika mahojiano na Fox News.

Alionya kuwa iwapo Tehran itaweka vikwazo katika njia hiyo ya baharini, “haitabaki na nchi.” Pia alisema kuwa Marekani inaweza kuchukua udhibiti wa njia hiyo ya maji na kutoza ushuru wake yenyewe.

Mwakilishi mkuu wa Iran katika mazungumzo hayo ambaye pia ni Spika wa Bunge, Mohammad Baqer Qalibaf, alipuuza vitisho hivyo akisema: “Je, hawafikirii kwamba kama vitisho vyao vingekuwa na athari yoyote, wasingekuwa katika hali hii ya kukata tamaa leo? Haijalishi watazungumza kiasi gani, sisi ndio tunaochukua hatua.”

Baadaye aliwaonya maafisa wa Marekani “kuwa waangalifu” katika matamshi yao na kusisitiza kuwa vikosi vya ulinzi vya Iran viko tayari kujibu hatua yoyote.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *