
Rais wa Somalia amelaani vikali kile hatua ya utawala wa Israel kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake, akiahidi “kukabiliana” na uwepo wowote wa kijeshi wa Israel katika eneo la Somalia la Somaliland ambalo limejitangazia uhuru.
Katika mahojiano siku ya Jumamosi, Hassan Sheikh Mohamud alisema hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutambua eneo lililojitenga la Somaliland kama taifa huru ni “kitendo cha kiholela, kilicho kinyume na misingi ya haki, na kisicho halali chini ya sheria za kimataifa.”
Somaliland ni eneo lililojitenga kaskazini-magharibi mwa Somalia, ambalo zamani lilikoloniwa na Uingereza. Licha ya tangazo la upande mmoja la kujitenga upande, eneo hilo bado linatambulika kimataifa kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Somalia.
Eneo hilo linashikilia nafasi nyeti kijiografia, likiwa karibu na mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafiri wa baharini duniani, yaani lango bahari la Babul Mandab na linaunganisha Pembe ya Afrika na Asia Magharibi.
Katika miaka ya karibuni, Somaliland imekuwa ikitafuta uungwaji mkono wa nje kwa kuimarisha uhusiano na Falme za Kiarabu (UAE), mshirika wa utawala wa Israel chini ya Makubaliano ya Abraham, pamoja na Taiwan, kwa lengo la kujipatia uhalali wa kimataifa nje ya mamlaka ya Mogadishu.
Hatua ya Israel imefuatia ripoti kuwa utawala huo uliwasiliana na wahusika ndani ya Somaliland kujadili uwezekano wa kulitumia eneo hilo kwa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wakati wa vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza,vita ambavyo vimeua zaidi ya Wapalestina 72,000 na kuwaacha wengine zaidi ya 172,000 wakiwa wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Ingawa maafisa wa Israel na Somaliland walikanusha ripoti hizo, afisa mmoja wa Somaliland aliliambia Shirika la Habari la Channel 12 la Israel mwezi Januari kuwa wazo la kambi ya kijeshi ya Israel “liko mezani na linajadiliwa,” huku utekelezaji wake ukihusishwa na masharti maalumu.
Serikali ya Somalia imeitaja hatua ya Israel kuitambua Somaliland kama hujuma ya moja kwa moja dhidi ya mamlaka yake. Msimamo huo umeungwa mkono na nchi nyingi za Afrika na Kiarabu. Serikali ya Somalia imemtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kubatilisha uamuzi huo.
Mohamud pia aliweka wazi kuwa Mogadishu haitakubali kabisa uwepo wowote wa kijeshi wa Israel katika ardhi ya Somalia: “Tutapigana kwa uwezo wetu. Bila shaka tutajilinda … na hilo linamaanisha tutakabiliana na vikosi vyovyote vya Israel vitakavyoingia, kwa sababu tunapinga hilo na hatutalikubali kamwe.”
Rais huyo amesisitiza kuwa matumizi ya nguvu ya Israel yanayoleta mauti kwa Wapalestina huko Gaza hayawezi kutenganishwa na yanayoendelea Somaliland, akisema yote mawili yanaakisi kudhoofika kwa misingi na vizuizi vya kimataifa vinavyopaswa kulinda amani na utu wa binadamu.