
KIKOSI cha KMC kinajindaa kushuka uwanjani jioni ya kesho Jumatano ikiwa wenyeji wa Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku ikiwa ni kama imekumbwa na mdudu mbaya, kwani licha ya kuanza vibaya msimu huu ikiburuza mkia kwa muda mrefu, pia inaongoza ‘ligi ndogo’ ya kujifunga.
KMC iliyopanda Ligi Kuu msimu wa 2018-2019 na kufanya kweli kwa kumaliza katika nafasi ya nne na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwa sasa ndio inayoongoza kwa kujifunga ikifanya hivyo mara tatu kupitia mechi 14 ilizocheza hadi sasa ikivuna pointi nane tu.
Kabla ya mechi za jana, Ligi Kuu ilikuwa zimeshachezwa jumla ya mechi 93 na kufungwa mabao 164, yakiwamo saba ya kujifunga, huku KMC ikiongoza kwa wachezaji wake watatu kujiweka katika harakati za kuokoa hatari langoni mwao.
Wachezaji watatu wa KMC waliojiweka na kuifanya timu hiyo kuwa kinara hadi sasa ni Ibrahim Nindi aliyekuwa wa kwanza kwa timu hiyo, lakini wa tatu kwa Ligi nzima ya msimu huu siku KMC ilipolala bao 1-0 mbele ya JKT Tanzania Novemba 21 mwaka jana.
Hance Masoud ndiye aliyekuwa wa pili KMC kujiweka mwenyewe wavuni dhidi ya TRA United Januari 23 mwaka huu na Wana Kinondoni kupasuka mabao 3-0 mjini Tabora kabla ya juzi tena, Ismail Gumbo kujifunga mbele ya Dodoma Jiji KMC ikifa 2-1.
Kwa mwaka huu pekee KMC imeshajiweka mara mbili na kuongoza orodha ya walijofunga ikifuatiwa na Pamba Jiji iliyojiweka kupitia James Mwashinga ilipolala 1-0 kwa Mtibwa Sugar.
KMC inayonolewa na kocha Abdallah Mohammed ‘Baresi’ kesho itakuwa mwenyeji wa Simba katika mechi ya kukamilisha duru la kwanza kwenye Uwanja wa KMC Complex, ikiwa imeshinda mechi mbili tu na kutoka sare mbili, huku ikipoteza 10 ikiwa kinara kwa timu zilizopoteza mechi nyingi.
Mbali na KMC na Pamba Jiji, timu nyingine zilizopo katika ‘ligi’ hiyo ndogo ya kujiweka ni Coastal Union iliyokuwa ya kwanza kujifunga dhidi ya Dodoma Jiji, Fountain Gate kupitia Lamela Maneno ipo katika orodha ilipojiweka mbele ya Mtibwa na Singida Black Stars ikikamilisha timu tano zilizojiweka hadi sasa wakati beki Anthony Tra Bi Tra alipojifunga mbele ya TRA United ilipofumuliwa kwa mabao 3-0 mwishoni mwa 2025.
Wakati KMC ikiongozwa kaatika orodha hiyo ya timu zilizojiweka, upande wa timu zilizonufaika na mabao ya kufungiwa ni TRA United, Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji ambazo kila moja imenufaika mara mbili na nyingine ni JKT Tanzania iliyofungiwa bao moja.
Pamba Jiji ndio timu pekee hadi sasa iliyonufaika kwa kupewa ushindi wa mezani dhidi ya Dodoma Jiji, ikivuna pointi tatu na mabao matatu katika mechi iliyoshindwa kumalizika kwa sababu ya tatizo la umeme Oktoba 25 mwaka jana.
Rekodi zinaonyesha msimu wa 2022-2023 ndio uliokuwa na mabao mengi ya kujifunga ambao wachezaji 20 walijiweka huku msimu uliopita wa 2024-2025 ukifuata (19).
Msimu wa 2023-2024 yalifungwa mabao 12 kwa msimu mzima. Msimu huu utaishaje kama hadi sasa yakiwa yameshawekwa saba kupitia mechi 93 tu? Tusubiri!