WAKATI dirisha la usajili la majira ya kiangazi likizidi kushika kasi barani Ulaya, jina la kiungo Mtanzania Lisa Baum limekuwa miongoni mwa yanayozungumzwa zaidi katika soka la wanawake kutokana na vita ya vigogo kadhaa wanaowania saini yake.

Baum, mwenye umri wa miaka 19 na aliyezaliwa Tanzania kabla ya familia yake kuhamia Ujerumani akiwa na miaka minne, ameibuka kuwa mmoja wa vipaji vinavyowindwa zaidi barani humo baada ya msimu mzuri akiwa na RB Leipzig.

Taarifa kutoka Ujerumani zinaeleza kuwa mabingwa wa Ulaya, Barcelona, ni miongoni mwa timu zinazomtazama zaidi winga huyo, huku Lyon, Manchester United, Bayern Munich na London City Lionesses nazo zikitajwa kuwa katika mbio hizo.

Hata hivyo, Arsenal ndiyo inayoonekana kuwa mbele zaidi katika harakati za kumshawishi nyota huyo kuhamia London kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

RB Leipzing wanahitaji kiasi cha zaidi ya Euro 550,000 (zaidi ya Sh1.7 bilioni). Kutokana na ushindani wa timu hizo RB Leipzig wana matumaini ya kuvunja rekodi ya uhamisho wa mchezaji huyo kutoka Bundesliga endapo wataamua kumuachia Lisa Baum katika dirisha hili la usajili.

Winga huyo mwenye umri wa miaka 19 anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wachache wa Bundesliga ya wanawake wenye uwezo wa kuvunja rekodi ya ada ya usajili kutokana na idadi ya vigogo wa Ulaya wanaomuwania kwa sasa.

Baum amejiunga na kundi la wachezaji wachanga wanaotazamwa kama nyota wa baadaye wa soka la wanawake barani Ulaya kutokana na kiwango alichoonyesha katika msimu wake wa kwanza akiwa na Leipzig.

Akiwa sehemu muhimu ya kikosi hicho, alicheza mechi 23 za ligi, akifunga mabao sita na kutoa pasi mbili za mabao, takwimu zilizomfanya kuwa mmoja wa wachezaji waliobeba matumaini ya klabu hiyo msimu uliopita.

Mbali na mabao na pasi za mwisho, Baum alivutia mashabiki kwa uwezo wake wa kupiga chenga, kasi kubwa akiwa na mpira na uwezo wa kuwapa wakati mgumu mabeki wa timu pinzani.

Ni sifa hizo zilizowafanya maskauti wa baadhi ya klabu kubwa zaidi duniani kuanza kufuatilia maendeleo yake kwa karibu.

Kuongezeka kwa idadi ya timu zinazomuhitaji kunaweza kuwa habari njema kwa Leipzig kwa sababu klabu hiyo ina nafasi ya kufanya biashara kubwa kutokana na thamani ya mchezaji huyo kuendelea kupanda.

Baum alijiunga na Leipzig akiwa mchezaji huru akitokea  Hamburger SV msimu uliopita, lakini sasa anatajwa kama mmoja wa wachezaji wenye thamani kubwa zaidi katika kikosi hicho kutokana na maendeleo aliyoyaonyesha ndani ya muda mfupi.

Kinachovutia zaidi ni kwamba pamoja na kuwindwa na vigogo hao wa Ulaya, Baum bado hajacheza mechi yoyote katika timu kubwa ya taifa ya wanawake ya Ujerumani.

“Lengo langu si kuwa staa, nataka zaidi kuwa na furaha na kile ninachokifanya,” alisema Baum akisisitiza umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya ustawi wake wa baadae.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *