Tabora. Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa zaidi ya Sh109 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme Awamu ya Pili B (HEP) utakaonufaisha vitongoji 660 katika wilaya saba za Mkoa wa Tabora.
Hatua hiyo imekuja wakati wa kuwatambulisha wakandarasi wawili, kampuni za Sinotec Limited na Namis Limited, ambao watatekeleza mradi huo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Akizungumza leo Februari 9, 2026 mara baada ya utambulisho wa wakandarasi na makabidhiano ya usimamizi wa mradi, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amewataka wakandarasi hao kufanya kazi kwa uadilifu, ubora na kwa kuzingatia muda uliopangwa.
Amesema Serikali haitakuwa na uvumilivu kwa wakandarasi wazembe au wanaochelewesha utekelezaji wa miradi kwa wananchi.
“Sitakuwa na uvumilivu kwa wakandarasi wazembe au wanaofanya kazi chini ya kiwango. Hilo hatulitaki kabisa,” amesema Chacha.
Wakandarasi pamoja na watumishi wengine mkoa wa Tabora wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Tabora, Paul Chacha.
Ameeleza kuwa kiasi kikubwa cha fedha kimetolewa kutokana na uhitaji mkubwa wa nishati mkoani humo, akisisitiza kuwa Tabora ni mkoa mkubwa hivyo hakuna nafasi ya uzembe.
“Haiwezekani mkandarasi apewe fedha na kazi halafu afanye uzembe. Mkifanya kazi vizuri, Serikali iko tayari hata kuongeza mkataba,” amesema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Musa Muze, amemuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutoa maeneo kwa ajili ya kupitisha nguzo za umeme na kuchukua hatua dhidi ya wanaoharibu miundombinu.
Amesema changamoto kubwa zinazowakabili wakandarasi ni uharibifu wa miundombinu pamoja na wananchi kukataa nguzo zipite katika maeneo yao, hali inayochelewesha utekelezaji wa miradi.
Pia amebainisha changamoto ya mwitikio mdogo wa wananchi kuunganisha umeme majumbani, licha ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.
“Serikali inawekeza fedha nyingi, lakini wananchi wanaunganisha umeme kwa kasi ndogo, jambo linalopunguza tija ya miradi,” amesema.
Meneja wa Usimamizi wa Miradi wa REA Mkoa wa Tabora, Oscar Benedicto, amesema mradi huo utatekelezwa kwa karibu na kukamilika kwa wakati uliopangwa.
“Tutausimamia kwa karibu kuhakikisha vitongoji vyote 660 vinafikiwa kama ilivyokusudiwa,” amesema.
Naye mwakilishi wa mkandarasi wa Sinotec Limited, Zhang Jianguang, amesema kampuni hiyo itakamilisha upembuzi yakinifu ndani ya miezi miwili na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Namis Limited, Shaidu Rukakolezibwa, amesema hakuna vikwazo vitakavyosababisha kuchelewa kwa mradi huo.
“Tuko tayari kufanya kazi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango,” amesema.
Takwimu zinaonyesha kuwa hadi mwaka 2025, Serikali imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyote 724 vya Mkoa wa Tabora na vitongoji 1,525 kati ya 3,749, sawa na asilimia 40.
Serikali imepanga kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.