
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watoto milioni 100 wameachishwa shule kutokana na migogoro.
Ripoti nya Umoja wa Mataifa inasema, idadi ya watoto na vijana ambao upatikanaji wao wa elimu umevurugwa kutokana na migogoro na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, imeongezeka na kufikia watu milioni 258.
Takriban watoto milioni 100 kati ya hao wamelazimika kuacha kabisa shule. Hii ni kulingana na ripoti iliyotolewa Jumanne na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Elimu Haiwezi Kusubiri (Education Cannot Wait) unaosimamia masuala ya elimu katika maeneo yenye migogoro.
Ripoti hiyo imeangazia watoto na vijana wenye umri wa kwenda shule ambao elimu yao imevurugwa na migogoro , kulazimika kuyahama makazi yao, athari za mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na migogoro ya kijamii na kiuchumi.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa watoto milioni 93 wameacha shule na kwamba karibu asilimia 60 ya watu milioni 258 walioathiriwa na kadhia hiyo wanaishi katika mataifa tisa ambayo ni Afghanistan, Bangladesh, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Myanmar, Nigeria, Pakistan, Sudan na Yemen.