Thamani mifuko hifadhi ya jamii yafikia tril 24/-Thamani mifuko hifadhi ya jamii yafikia tril 24/-

SERIKALI imesema thamani ya mifuko ya hifadhi ya jamii imeongezeka kutoka Sh trilioni 10.43 mwaka 2020 hadi Sh trilioni 24.20 Desemba mwaka jana.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu alisema hayo alipozungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa sekta ya kinga ya jamii jijini
Arusha.

Sangu alisema ukuaji huo ni matokeo ya maboresho ya kisera na kisheria yaliyofanyika kuanzia mwaka 2018.

Alisema idadi ya wanachama katika mifuko ya PSSSF na NSSF imeongezeka kwa asilimia 106 ndani ya miaka mitano na uwekezaji wa mifuko hiyo ukifikia Sh trilioni 20.13 katika maeneo mbalimbali zikiwemo hati fungani za serikali, miliki ardhi na hisa.

Sangu alisema mafanikio hayo yameenda sambamba na uimarishaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao katika awamu ya pili umenufaisha zaidi ya kaya milioni 1.37 zenye takribani watu milioni 5.5 kwa ruzuku ya zaidi ya Sh trilioni 1.55.

Alisema katika awamu ya kwanza ulinufaisha kaya milioni 1.1 kwa kuwapatia huduma zenye thamani ya Sh bilioni 968.

Sangu alisema tathmini iliyofanyika mwaka 2013 iliwezesha kuanza kutekelezwa kwa Mpango wa Awamu ya Pili ulioanza mwaka 2020 hadi Septemba mwaka jana.

Alisema kupitia mpango huo zaidi ya kaya milioni 1.37 zenye takribani watu milioni 5.5 zimenufaika.

Sangu alisema katika kipindi hicho serikali ilitoa zaidi ya Sh trilioni 1.55 ikiwa ni ruzuku kwa kaya za walengwa sambamba na kuimarisha mpango wa ajira za muda ulionufaisha zaidi ya walengwa 600,000 kwa ujira wa zaidi ya Sh bilioni 214.

Alisema serikali itaendelea kutekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini ikiwa ni hatua muhimu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii na Dira 2050.

Sangu alisisitiza dhamira ya serikali ya kuendelea kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia utafiti wa namna ya kugharamia kinga ya jamii isiyo ya uchangiaji kwa kushirikiana na Tasaf.

Sera ya kinga ya jamii Sangu alizindua Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya Mwaka 2023 na Skimu ya Wananchi Waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi.

Uzinduzi huo unalenga kuwajumuisha wakulima, wafugaji na wajasiriamali wadogo katika mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii ili kupata kinga dhidi ya majanga kama uzee na ulemavu.

Kupitia sera hiyo serikali inalenga kuweka uratibu na mfumo imara wa ugharimiaji unaojumuisha kinga ya jamii ya uchangiaji kupitia mifuko ya NSSF, PSSSF na WCF na programu za misaada ya kijamii zisizo za uchangiaji kwa ajili ya kaya zilizo katika mazingira magumu.

Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 imekuja na mwelekeo wa kisasa unaolenga kuongeza wigo wa huduma hizi kwa makundi ambayo kwa muda mrefu yamesahaulika tangu nchi ipate uhuru.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ,Kazi, Ajira na Mahusiano, Mary Maganga alisema uzinduzi wa sera hizo ni chachu ya maendeleo ya jamii kwa kuwa unahusisha makundi ya uchangiaji, yasiyo ya uchangiaji, jumuishi na ustawi wa jamii Maboresho yaliyofanyika kuanzia mwaka 2018 yaliifanya NSSF kuwa mfuko pekee wenye jukumu la kuhudumia wananchi waliojiajiri, ambao wanajumuisha zaidi ya asilimia 80 ya nguvukazi ya taifa.

Katika kutekeleza azma hiyo, NSSF imeanzisha Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi wanaojiajiri katika  sekta isiyo rasmi, maarufu kama Hifadhi Skimu, ambayo imesanifiwa kulingana na mazingira ya vipato vya walengwa.

Skimu hiyo inawawezesha wanachama waliojiajiri kwenye sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa
madini, sanaa, bodaboda na biashara ndogo ndogo kujichangia fedha kidogo kidogo kulingana na vipato vyao kupitia mifumo rahisi ya kidijiti zikiwemo simu za kiganjani, benki na mawakala wa fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *