
Nchini DRC, ujumbe wa Umoja wa Mataifa unajiandaa kwa ajili ya kuanza tena shughuli zake hatu kwa hatua huko Kivu Kusini, ametangaza Jean-Pierre Lacroix siku ya Jumanne.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Kinshasa, Paulina Zidi
Mkuu wa Operesheni za kikosi cha Umoja wa Mataifa anazuru nchi hiyo kwa sasa. Amepangwa kusafiri hadi Beni, makao makuu ya MONUSCO mashariki, leo Jumatano. Kabla ya hapo, alikutana na Rais Félix Tshisekedi siku ya Jumanne asubuhi kujadili jukumu la MONUSCO katika utaratibu wa uthibitishaji wa kusitisha mapigano. Ni ndani ya mfumo huu ambapo ujumbe huo utahamishiwa Kivu Kusini, kuanzia na Uvira. Uliondoka kutoka mkoa huo wa Kivu Kusini mnamo mwaka wa 2024.
Kutumwa kwa wanajeshi wa MONUSCO kwenda Uvira kutafanyika katika hatua kadhaa, Jean-Pierre Lacroix alieleza. Kwanza, kutakuwa na upelelezi wa angani ili kuchora ramani ya eneo hilo. Kwa lengo hilo, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alieleza: “Tunahitaji dhamana za usalama.”
“Hatutatuma helikopta zetu ziruke na wafanyakazi wetu, kutokana na hatari ya matukio kama yaliyotokea, au hatari ya ndege zisizo na rubani katika maeneo ya karibu. Hili ni jambo la lazima, jambo ambalo tumeomba. Na kwa kuwa nilikutana na wawakilishi wa mabalozi wa nchi za kigeni siku ya Jumanne, pia niliomba msaada wao ili tuweze kupata dhamana hizi haraka iwezekanavyo. Hili ni sharti la harakati ya awali kuelekea Uvira,” Jean-Pierre Lacroix alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia aliongeza kwamba safari hizi za ndege za upelelezi lazima ziondoke Goma, eneo ambalo kwa sasa linakaliwa na kundi lenye silaha la AFC/M23, ambalo uwanja wake wa ndege umefungwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Kufuatia safari zake za upelelezi, kupelekwa kwa wanajeshi wa ardhini kutazingatiwa. Kwanza idadi itapunguzwa, kabla ya kuongezwa. Hata hivyo, Jean-Pierre Lacroix anabainisha kwamba Umoja wa Mataifa pekee hauwezi kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyosainiwa Washington na Doha. Kwa hivyo, ahadi ya kidiplomasia ya wadhamini wao, Marekani na Qatar, ni muhimu.