DAR ES SALAAM: Mjasiriamali wa Kitanzania anayeishi diaspora, Chris Lukosi, amesema mafanikio ya biashara hayawezi kutenganishwa na wajibu kwa jamii, akieleza kuwa ajira, ulipaji wa kodi na misaada kwa wenye uhitaji ni sehemu ya msingi ya falsafa yake ya uongozi wa kibiashara.
Kupitia shughuli zake za minada, uingizaji wa bidhaa kutoka Ulaya na miradi ya ujenzi, Lukosi anasema ameajiri moja kwa moja mamia ya vijana na kuchochea ajira zisizo za moja kwa moja katika sekta za usafirishaji, ulinzi binafsi, upakuaji mizigo, mauzo na huduma za kiufundi.
“Kila mafanikio yana wajibu,” alisema Lukosi katika mahojiano. “Mungu amenipa nafasi, na ninaamini nina jukumu la kusaidia wale ambao hawajapata fursa kama mimi.”
Kwa mujibu wa Lukosi, kila kontena linaloingia nchini linahusisha mnyororo wa ajira — kuanzia bandarini hadi kwenye soko la mwisho. Anasema mchango huo hauishii kwenye biashara pekee bali pia kwenye mapato ya kodi kwa serikali.

“Unapoleta mzigo, kuna ushuru, kuna ajira, kuna mauzo. Huo ndio mchango wangu kwa taifa,” alisema. “Ninajivunia kuchangia pato la taifa.”
Mbali na ajira, Lukosi amesema amekuwa akisaidia familia zenye uhitaji kwa kulipia kodi za nyumba, kusafirisha bidhaa za msaada na kugawa vifaa vya matumizi ya kila siku. Anasisitiza kuwa misaada hiyo hufanyika kwa uwazi na kwa lengo la kusaidia, si kujitangaza.
“Sio lazima uwe kanisani kila siku kuonyesha imani yako,” alisema. “Kwangu kusaidia ni ibada.”
Wachambuzi wa maendeleo ya jamii wanasema mtazamo huo unaendana na dhana ya corporate social responsibility (CSR), ambapo sekta binafsi ina jukumu la kuimarisha ustawi wa jamii inayozunguka biashara zao. Hata hivyo, wataalam wanaonya kuwa msaada wa kijamii unahitaji kuwa endelevu na wa kimkakati ili kuleta mabadiliko ya muda mrefu.
Lukosi anasema dhamira yake si kutoa msaada wa muda mfupi pekee, bali kuweka mazingira yanayowawezesha vijana kujiajiri na kukuza biashara zao kupitia minada na fursa za usambazaji bidhaa.
“Biashara bila jamii haina maana,” alisema. “Nataka vijana wapate fursa, wasimame kwa miguu yao.”
Anasema uzoefu wake binafsi wa kupitia changamoto za kifedha ulimfanya kuelewa umuhimu wa kusaidiwa katika nyakati ngumu. “Nilipitia nyakati ambazo msaada mdogo ungeweza kubadilisha maisha yangu,” alisema na kuongeza:
“Leo nikiwa na uwezo, ninaona ni wajibu wangu kufanya hivyo kwa wengine.”
Kwa mujibu wa wachambuzi wa uchumi, mchango wa wafanyabiashara wanaorejesha sehemu ya mapato yao kwa jamii unaweza kusaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kuimarisha uhusiano kati ya sekta binafsi na wananchi.