
Shirika la afya duniani WHO linaonya kuwa maambukizi ya virusi hatari vya ugonjwa wa Ebola, yanaendelea kusambaa kwa kasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, licha ya kuwepo kwa jitihada za kupambana na ugongwa huo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mkuu wa WHO Marie-Roseline Belizaire, anayehusika na misaada ya dharura barani Afrika amesema hali inaendelea kuwa mbaya, hasa maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa DRC.
Mpaka sasa, tangu virusi hivyo vya Ebola aina ya Bundibugyo ambavyo havina dawa wala chanjo, vimewambukiza watu 896, huku watu 232 wakithibitishwa kupoteza maisha.
Watu wengine 21 wamethibitishwa kuambukizwa kwa muda wa saa 24 zilizopita. Aidha, WHO inasema maafisa wa afya 75 nchini DRC wameambukizwa Ebola na 17 kati yao wamepoteza maisha tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipotangazwa Mei tarehe 15.
Maambukizi kwa watalaam wa afya inaelezwa kuwa yalitokana na uhaba wa vifaa vya kujikinga na ukosefu mkubwa wa wahudumu wa afya katika maeneo yalioripotiwa ugonjwa huo.
Jimbo la Ituri ndilo lililoathiriwa zaidi, ambapo ina asilimia 90 ya maambukizi yote. Katika nchi Jirani ya Uganda, WHO inasema kwa siku 12 zilizopita, hakuna maambukizi mapya yaliyoripotiwa, baada ya kuripotiwa kwa wagonjwa 19, kati yao wawili walipoteza maisha na 10 walipona.