Duniani kote, pengo kubwa la kijinsia bado linaendelea katika ngazi zote za taaluma za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kutokana na ukosefu wa ufadhili wa utafiti, mitazamo ya kijinsia iliyozoeleka, na vitendo vya ubaguzi mahali pa kazi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema pengo hilo linaonekana zaidi katika sekta ya teknolojia, ambapo wanawake wanawakilisha asilimia 26 tu ya nguvu kazi katika data na akili Mnemba (AI), na asilimia 12 tu katika masuala ya kompyuta au cloud computing.

Ameonya kuwa “Kuondoa wanawake katika sayansi kunadhoofisha uwezo wetu wa pamoja wa kukabiliana na changamoto za haraka za kimataifa, kuanzia mabadiliko ya tabianchi hadi afya ya umma na usalama wa anga za juu”.

Sarah Ehab Nagaty Abdelkader, mtaalamu wa Shahada ya Uzamivu katika taasisi ya afya ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Marekani mjini Cairo. Alishinda tuzo ya L'Oréal-UNESCO Kwa Wanawake katika Sayansi ya Vijana Wenye Vipaji.

Sarah Abdelkader

Sarah Ehab Nagaty Abdelkader, mtaalamu wa Shahada ya Uzamivu katika taasisi ya afya ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Marekani mjini Cairo. Alishinda tuzo ya L’Oréal-UNESCO Kwa Wanawake katika Sayansi ya Vijana Wenye Vipaji.

Ushirikishwaji mkubwa zaidi

Wakati jamii zikiendelea kukabiliana na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, Umoja wa Mataifa unaamini kuwa kuunganisha akili mnemba AI, sayansi ya jamii, STEM na fedha kunatoa njia ya kuharakisha maendeleo jumuishi na endelevu.

Mbinu hii inaangaziwa leo katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, inayoadhimishwa kila mwaka Februari 11.

Kuleta pamoja nyanja hizi nne kunaweza kusaidia kuvunja vikwazo vinavyoendelea kwa kuziba pengo la kijinsia katika ujuzi wa kidijitali, kuchochea uanzishwaji wa biashara zinazoongozwa na wanawake, kuendeleza usimamizi wa AI unaozingatia usawa wa kijinsia, na kuhamasisha fedha kwa ujumuishaji wa kijamii kama kipimo cha utendaji.

“Kuanzia kuendeleza nishati jadidifu hadi kuzuia majanga yajayo mustakabali wetu unategemea kufungua na kutumia vipaji vya binadamu kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo,” amesema Katibu Mkuu.

Guterres ameongeza kuwa “Leo na kila siku, tuhakikishe kwamba wanawake na wasichana wanaweza kutimiza ndoto zao za kisayansi kwa haki zao, na kwa manufaa ya wote.”

Mwanasayansi wa kike aliyevaa miwani ya usalama na koti la maabara anashikilia chupa ndogo ya kupima katika mazingira ya maabara.

© University of Bath

Mwanasayansi wa Kike katika Maabara Kushikilia Chupa ya Mtihani

Mwanasayansi, mjasiriamali, balozi

Mwanakemia na mjasiriamali Asel Sartbaeva kutoka Kyrgyzstan ni mfano bora katika eneo hili.

Yeye ni Profesa Msaidizi wa Kemia katika Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza, na mwanzilishi mwenza pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya bioteknolojia ya EnsiliTech.

Kazi yake inashughulikia moja ya changamoto sugu katika afya ya kimataifa, jinsi ya kufanya chanjo ziwe thabiti katika joto la kiwango cha juu ili ziweze kusafirishwa hadi katika jamii za mbali bila kuhitaji mifumo tata ya ubaridi.

Kuwasaidia wasichana katika STEM

Mbali na utafiti wake, Bi. Sartbaeva anashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, kama balozi wa mpango wa Wasichana katika Sayansi nchini Kyrgyzstan, akihamasisha wasichana kujiunga na elimu ya juu na taaluma za STEM.

Ameiambia UN News kwamba katika jamii nyingi, maamuzi kuhusu mustakabali wa msichana huathiriwa na familia yake  hasa baba yake.

“Mara nyingi, hofu kubwa niliyosikia, hasa kutoka kwa akina baba, ni kwamba walidhani kuwa wasichana wao wakiingia katika sayansi hawataweza kuwa na familia,” amesema.

“Kwangu mimi, jambo la kwanza lilikuwa kuonesha kwamba hilo si kweli. Wanaweza kuwa na vyote viwili, na mambo hayo hayapingani.”

media:entermedia_image:775d887e-21b8-423b-aff8-e72b8abf6df3

UN Photo/Loey Felipe

Kuinua Wanawake katika masomo ya STEM kwenye Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi. (Maktaba)

Tunakuhitaji

Mpango wa UNICEF unajumuisha madarasa maalum ya sayansi, ushauri elekezi, mafunzo ya mawasiliano na kujenga kujiamini. 

Maelfu ya wasichana wameshiriki, na wengi wao wameendelea kusomea shahada za vyuo vikuu katika taaluma za STEM.

Bi. Sartbaeva anaamini kuwa fursa kwa wanawake katika sayansi zinaimarika. Wakati alipokuwa chuoni, maprofesa wanawake walikuwa wachache, lakini leo anaona uwiano bora zaidi na sera madhubuti zinazounga mkono ujumuishaji.

Hata hivyo, bado kunahitajika vipaji zaidi, na ana ujumbe mmoja wazi na rahisi kwa wasichana wanaofikiria kuingia katika STEM, “Tunakuhitaji”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *