Dar es Salaam. Gharama kubwa za upasuaji wa magonjwa ya moyo kwa watoto zinazofikia kati ya Sh8 milioni na Sh20 milioni kwa mgonjwa mmoja, zimeendelea kuwa kikwazo kwa familia nyingi zenye kipato cha chini, huku takribani watoto 4,000 nchini wakihitaji huduma hiyo kila mwaka ili kuokoa maisha yao.

Hata hivyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imewahakikishia wazazi kuwa hakuna mtoto atakayekosa matibabu kutokana na ukosefu wa fedha.

Taasisi hiyo imesema inaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wote wanaohitaji upasuaji wanapatiwa huduma.

Akizungumza leo Ijumaa Juni 26, 2026 wakati wa kupokea msaada wa Sh20 milioni kutoka Benki ya KCB Tanzania kwa ajili ya kugharamia upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema gharama za matibabu ya moyo kwa watoto bado ni changamoto kubwa kwa familia nyingi, hasa zenye kipato cha chini.

Amesema licha ya Serikali kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya kisasa, vifaa tiba na wataalamu wa upasuaji wa moyo, uwezo mdogo wa kifedha wa baadhi ya familia umeendelea kuwa kikwazo kwa watoto kupata huduma kwa wakati.

Kwa mujibu wa Dk Kisenge, Serikali kwa sasa hugharamia zaidi ya asilimia 70 ya matibabu hayo, huku sehemu iliyobaki ikigharamiwa kupitia michango ya wadau na wahisani.

“Gharama za upasuaji ni kati ya Sh8 milioni hadi Sh20 milioni. Hata kwa mtu mwenye ajira rasmi si fedha ndogo, sembuse mzazi wa kipato cha chini. Hii ndiyo sababu tunashirikiana na wadau kuhakikisha mtoto anayefika JKCI hakosi nafasi ya kutibiwa kwa sababu ya fedha,” amesema.

Kutokana na changamoto hiyo, amesema JKCI imeanzisha Heart Team Foundation, ambayo inaratibu upatikanaji wa fedha kutoka kwa wadau mbalimbali ili kusaidia watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo kugharamia matibabu yao.

Amewahakikishia wazazi kuwa hakuna mtoto atakayekosa upasuaji kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama, mradi taratibu zilizowekwa na taasisi hiyo zifuatwe.

“Nataka kuwatoa hofu wazazi wote. Hakuna mtoto atakayeshindwa kufanyiwa upasuaji kwa sababu ya kukosa fedha, mradi taratibu zilizowekwa zifuatwe. Dhamira yetu ni kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kuishi na kuwa sehemu ya taifa la kesho,” amesema.

Wakati huo huo, Dk Kisenge amesema takwimu zinaonyesha duniani watoto sita hadi wanane kati ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa huwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo.

Amesema kwa Tanzania huzaliwa zaidi ya watoto milioni mbili kila mwaka, huku makadirio yakionyesha zaidi ya watoto 12,000 huzaliwa na matatizo ya moyo na kati yao, takribani 4,000 huhitaji kufanyiwa upasuaji.

“Tanzania huzaliwa watoto zaidi ya milioni mbili kwa mwaka. Kwa takwimu hizo tunakadiria kuwa zaidi ya watoto 12,000 huzaliwa na matatizo ya moyo na kati yao takribani 4,000 huhitaji kufanyiwa upasuaji,” amesema.

Ametaja baadhi ya sababu za watoto kupata magonjwa ya moyo kuwa ni matatizo ya kuzaliwa nayo yanayotokana na vinasaba, matumizi ya pombe na sigara wakati wa ujauzito, lishe duni kwa mama mjamzito pamoja na maambukizi yanayoweza kuharibu valvu za moyo mtoto anapokuwa anakua.

Aidha, amesema baadhi ya watoto hupata maambukizi ya bakteria yanayoharibu valvu za moyo, hali inayohitaji matibabu ya haraka ili kuzuia madhara makubwa zaidi.

KCB yatoa Sh20 milioni

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Angelina Semiono amesema benki hiyo imetoa Sh20 milioni kwa JKCI ili kusaidia kugharamia upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo pamoja na matibabu yao baada ya upasuaji.

Amesema uamuzi wa kutoa msaada huo umetokana na kutambua kuwa gharama za matibabu hayo ni kubwa na zinazozidi uwezo wa familia nyingi.

“Tunaamini kila mtoto anastahili nafasi ya kuishi. Thamani ya mchango wetu haipimwi kwa kiasi cha fedha tulichotoa, bali kwa maisha yatakayookolewa na fursa mpya ambazo watoto hawa watapata baada ya kupona,” amesema.

Amesisitiza kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana kwa juhudi za taasisi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Naye Anna Jasper, aliyezungumza kwa niaba ya wazazi walionufaika na msamaha wa matibabu kutoka JKCI, amewashukuru wadau wanaoendelea kuchangia huduma hizo na kuwataka wengine kujitokeza ili watoto wengi zaidi wenye magonjwa ya moyo wapate matibabu na kuendelea kuishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *