Zanzibar. Ule msemo wa ng’ombe hazeeki maini, siyo uongo. Unadhihirishwa na mwanamuziki, mwandishi, na Mkurugenzi wa United African Alliance Community Centre (UAACC), Charlotte Hill O’Neal, ‘Mama C ambaye licha ya kuwa na umri wa miaka 75 bado analitumikia jukwaa ipasavyo.
Akiwa kati ya wasanii waliotumbuiza kwenye tamasha la Sauti za Busara 2026, lilifanyika Zanzibar kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Mama C anaeleza siri ya ushujaa wake jukwaani.
“Inanishangaza kwamba bado ninaweza kufanya mambo kama haya. Ninapata furaha kubwa sana kufanya kazi na vijana na watoto pia, kwa sababu tunawapa nafasi waangaze nuru yao wenyewe.
“Wanapochukuliwa kama wasanii, wanapata kujiamini katika kila wanachofanya. Ndiyo maana sanaa, muziki, sanaa za picha, mashairi vyote ni muhimu sana. Vinainua ari ya vijana na kuwawezesha kung’aa,”anasema
Aidha Mama C anamtaja mume wake Pete O’Neill kama sababu ya ushujaa jukwaani hadi sasa.
“Jambo moja ni mume wangu, Pete O’Neill, ambaye nimekuwa naye kwenye ndoa kwa miaka 57. Ananipa ujasiri. Ananipa ruhusa ingawa sihitaji ruhusa ya kuacha kipaji changu,”amesema
Akizungumzia wasanii wa kizazi kipya, anasema ni vizuri wajitambue wao wenyewe kupitia sanaa.
“Ni vizuri kuheshimu tamaduni zetu. Unajua tamaduni za Tanzania? Afrika nzima, diaspora kote duniani, kwa sababu sisi Waafrika tupo kila mahali. Tunapaswa kuukumbatia muziki wetu, mila zetu, lugha zetu na tamaduni zetu.
“Hilo ni jambo muhimu sana kwa vijana ili wawe na mwanga wao na waangaze. Nami nahisi bado ninaangaza baada ya miaka yote hii. Bado nina mng’ao huo,”anasema Mama C
Hata hivyo, hakuwaacha nyuma vijana wanaopambania ndoto zao kwa kuwashauri, watambue nguvu walizonazo.
“Nadhani kizazi cha sasa na kinachokuja kinahitaji kutambua nguvu walizonazo za kuubadilisha ulimwengu kupitia maneno yao. Kupitia muziki wao, kupitia vibe yao, hilo ni muhimu sana.
Katika muziki wetu, mara zote tunazungumzia upendo kwa sababu ni moja ya mambo muhimu zaidi duniani.
“Tunapenda kile tunachokifanya. Hilo ndilo nawaomba wakumbuke kushirikisha upendo huo, kujithamini wao wenyewe na kujenga umoja kati ya ndugu na watu wote duniani,”anasema
Akizungumzia muziki unavyoweza kuwa sehemu ya mabadiliko ya kupinga ukatili. anasema watu hukosa ujasiri wa kuzungumzia mambo nyeti yanayohitaji kubadilika.
“Tunaweza kufanya hivyo kupitia mashairi yetu, kupitia beti za hip-hop ambazo ni mashairi kupitia muziki wetu. Hapo tunapata ujasiri wa kuzungumzia mambo yenye maana, mambo yanayoweza kubadilisha jamii zetu kuanzia vijijini hadi ngazi za juu za serikali.
“Watu wanaweza kujifunza kutoka kwenye ujumbe wetu na kuishi kwa kile tunachokiita kwa Kiyoruba Iwa Pẹlẹ maana yake ni tabia njema na upole na kuwa mfano wa kile kinachowezekana, ili vijana wetu waweze kuangaza,”anasema
Kuhusu Sauti za Busara
“Nimeipenda sana. Nimeupenda mzuka wake wote. Nimefurahi kupata fursa ya kuleta vibe yetu Zanzibar. Nimefurahi mno. Sauti za Busara ni ya kipekee sana kwa sababu kuna watu kutoka sehemu mbalimbali duniani.
“Kuna aina zote za muziki, kama sisi tunavyotoka Arusha na tunachanganya blues, ala za jadi, hip-hop na vingine vyote kuwa kifurushi kimoja, na kila mtu akapenda. Tunaimba na kupiga muziki kutoka moyoni na ndani ya nafsi zetu, na hilo ndilo linalotufanya tutoe jasho jingi jukwaani,”anasema Mama C