Uzoefu wao unaangazia ujumbe mpana zaidi: ukuaji wa uchumi jumuishi unategemea kufungua nafasi kwa wale ambao mara nyingi hutengwa, wakiwemo watu wenye ulemavu, vijana na wabunifu wa nyumbani.

Mazingira yamlazimu kuwa mjasiriamali

Kwa Shaymaa Saeed, mbunifu mchanga wa kutumia sindano kufuma kwa kutumia nyuzi za sweta na msanii wa kazi za mikono kutoka Misri mwenye ulemavu, ujasiriamali haukuwa chaguo la mtindo wa maisha bali ni ulazima. Changamoto za kiafya zilimzuia kupata ajira rasmi, jambo lililomsukuma kutafakari upya jinsi ya kujipatia kipato.

“Mwaka 2018 nilianzisha mradi wangu nikiwa nyumbani kutokana na changamoto za kiafya, baada ya kushindwa kupata kazi,” ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa ya kiarabu huko Manama nchini Bahrain kunakofanyika  Jukwaa la Sita la Uwekezaji la Wajasiriamali Duniani (WEIF) linalofanyika wiki hii katika mji mkuu wa Bahrain, Manama, ambapo maonesho kuhusu ujasiriamali wa majumbani yanaonesha jinsi msaada mahsusi unaweza kubadilisha changamoto binafsi kuwa fursa za kiuchumi.

Amesema “badala ya kukata tamaa, niligeuza kipaji changu kuwa chanzo cha mapato.”

Jukwaa hilo limeandaliwa na Ofisi ya Kimataifa ya Uendelezaji wa Teknolojia na Ubunifu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) nchini Bahrain

Kilichoanza kama njia binafsi ya kukabiliana na hali hiyo, polepole kilikua na kuwa biashara inayoweza kujiendesha. Bi. Saeed ameshiriki katika baadhi ya maonesho makubwa zaidi ya kazi za mikono nchini Misri, akijenga kujiamini na kujulikana njiani.

Hivi karibuni, aliwasilisha kazi zake nje ya nchi yake kwa mara ya kwanza, hatua muhimu katika safari yake.

Kupanda jukwaani

“Ushiriki wangu unaashiria hatua yangu ya kwanza kwenye jukwaa la kimataifa,” amesema, akisisitiza nafasi ya mafunzo ya ujasiriamali na msaada wa taasisi. “Msaada nilioupata ulinisaidia kukua binafsi na kitaaluma, kwa kujiamini zaidi.”

Shaymaa Saeed, mwanamke mchanga wa Misri mwenye ulemavu na mtengenezaji wa crochet, anatabasamu wakati akionyesha vitu vyake vilivyotengenezwa kwa mikono kwenye hafla ya WEIF2026 huko Bahrain.

Habari za UN/Abdul Monem Makki

Shaymaa Saeed, mjasiriamali kijana wa Misri ambaye anahudhuria WEIF nchini Bahrain.

Jukwaa hili linawakutanisha wajasiriamali, watunga sera na wawekezaji kutoka nchi kadhaa.

Ndoto kubwa

Bi. Saeed bado anaendesha biashara yake yote akiwa nyumbani na mtandaoni, lakini ndoto zake zinaenda mbali zaidi. “Bado sina duka halisi, lakini nina ndoto ya kuwa na nafasi yangu mwenyewe ya kuonesha na kuuza kazi zangu, na kufikia masoko duniani kote kama biashara ndogo iliyofanikiwa.”

Yuko wazi kuhusu uhalisia wa kujenga biashara kutoka mwanzo. “Mafanikio hayaji mara moja,” amesema. “Ni safari endelevu ya juhudi, kujifunza na maendeleo.”

Mada zinazofanana zinaibuka kutoka kwa wanawake wengine wanaotumia sanaa na ujasiriamali kama njia za kujitambua na kujieleza.

Msemaji akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Uwekezaji wa Wajasiriamali Ulimwenguni 2026 huko Manama, Bahrain, na skrini kubwa inayoonyesha nembo za hafla hiyo na Malengo ya Maendeleo Endelevu.

UN News/Abdelmonem Makki

Msemaji katika World Entrepreneurs Investment Forum 2026 huko Manama, Bahrain.

Sanaa huzungumza pale lugha inaposhindwa

Msanii wa sanaa za kuona na mwalimu wa sanaa kutoka Bahrain, Mariam Sayed Anwar, ambaye pia ana ulemavu, ameelezea ubunifu kama nidhamu na pia njia ya kuachilia hisia.

“Kazi yangu inahusisha picha za vitu tulivu, michoro ya sura za watu, makaa ya kuchorea, penseli na rangi za akriliki,” amefafanua, akisisitiza umuhimu wa majaribio. “Sijiwekei mipaka kwa mbinu moja tu.”

Kwake, sanaa husema pale lugha inaposhindwa. “Kupitia rangi na brashi, naweza kueleza yaliyo moyoni na rohoni mwangu zaidi kuliko maandishi yanavyoweza. Sanaa ni lugha yangu; maneno yanaponyamaza, kazi yangu hunisemea.”

Uzoefu wa kimataifa wafungua macho wajasiriamali

Mbali na simulizi binafsi, wajasiriamali kutoka Afrika waliokusanyika Bahrain wanaangazia hali za kimuundo zinazochangia mafanikio au kushindwa.

Mjasiriamali kutoka Zimbabwe, Dkt. Roselyn Musaruru-Wacharewa, amesema kuunganishwa na mitandao ya kimataifa kumebadilisha mtazamo wake kuhusu kile kinachowezekana — si tu kwa wanawake binafsi, bali kwa maeneo mazima.

Katika nchi nyingi za Afrika, serikali huwatoza wajasiriamali kodi kubwa kiasi kwamba inaonekana kama zinataka utoke kabisa kwenye biashara,” amesema, akilinganisha na mazingira ambako sera zinahamasisha biashara kikamilifu.

Wito wake ulikuwa wa moja kwa moja: wanawake wajasiriamali wa Afrika wako tayari, lakini serikali lazima “zibadilishe simulizi na kuwapa fursa halisi na kutambuliwa.”

Dkt Roselyn Musaruru-Wacharewa, mjasiriamali kutoka Zimbabwe, anatabasamu katika hafla ya wataalamu huko Bahrain wakati wa WEIF 2026, akionyesha uzoefu wake na majukwaa ya biashara ya kimataifa.

Habari za UN/Abdul Monem Makki

Kutoka Zimbabwe, mjasiriamali Dr. Roselyn Musaruru-Wacharewa kutoka Zimbabwe alielezea jinsi kuonana na majukwaa ya kimataifa huko Bahrain kulivyobadilisha mtazamo wake.

Guterres asisitiza nafasi ya sekta binafsi

Umuhimu wa kuunda mazingira wezeshi kama hayo umesisitizwa pia na viongozi wa Umoja wa Mataifa na maafisa wa kitaifa, huku mkazo ukiwekwa kwenye matokeo badala ya maneno matupu.

Katika ujumbe wake uliowasilishwa Bahrain Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza nafasi ya sekta binafsi kama chachu ya ajira, ubunifu na uwekezaji, hasa kupitia biashara ndogo, za kati na ndogo sana, ambazo zinachangia takriban theluthi mbili ya ajira duniani.

ameeleza kuwa ukuaji lazima uende sambamba na heshima kwa haki za binadamu na viwango vya kazi, pamoja na kupanua fursa kwa wale waliobaki nyuma.

Maafisa wa UNIDO wameangazia vijana na wanawake kama nguzo kuu za ubunifu, huku mamlaka za Bahrain zikirejelea mipango ya kitaifa inayowaunga mkono vijana na wanawake wajasiriamali, pamoja na mikakati inayokumbatia akili bandia na teknolojia mpya.

Uzoefu halisi wa maisha

Hata hivyo, hoja zenye nguvu zaidi kuhusu ukuaji jumuishi hazikutoka kwenye kauli za sera, bali kutoka katika uzoefu halisi wa maisha.

Kuanzia biashara za nyumbani zinazoendeshwa kikamilifu mtandaoni hadi sanaa inayosema pale maneno yanaposhindwa, wajasiriamali kama Shaymaa Saeed wanaonyesha kile kinachowezekana pale vipaji vinapokutana na fursa — na kile kinachopotea pale vikwazo vinapoendelea kuwepo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *