Kila tarehe 13 Februari huadhimishwa Siku ya Redio Duniani, maadhimisho yanayokumbusha siku ambayo Redio ya Umoja wa Mataifa ilianza kurusha matangazo yake kwa mara ya kwanza miaka 80 iliyopita.

Timu za UN News zimekusanya simulizi kutoka pembe mbalimbali za dunia zinazoonesha ukweli mmoja rahisi, katika maeneo yaliyogawanywa na migogoro, majanga au pengo kubwa la kidijitali, redio hubaki kuwa sauti thabiti na ya kuaminika ikipeleka taarifa, faraja na muunganiko pale ambapo mawimbi mengine hayawezi kufika.

Kutoka Redio ya UM hadi UN News

Jukumu hili la kudumu limejengeka ndani ya historia ya Umoja wa Mataifa. Miaka 80 iliyopita, dunia ilipotoka katika uharibifu wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Redio ya Umoja wa Mataifa ilianza kurusha matangazo kutoka studio ndogo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifajijini New York, ikifikia hadhira kwa vipindi vya habari na makala maalum katika lugha tano, mara nyingi ikirusha moja kwa moja mijadala yote ya Baraza la Usalama.

Wafanyakazi wa Idara ya Redio ya Umoja wa Mataifa. wanafanya rekodi ya matangazo ya pekee kwa ajili ya mitandao ya redio ya nchi za Amerika ya Latini, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York.

UN Photo/MB

Wafanyakazi wa Idara ya Redio ya Umoja wa Mataifa. wanafanya rekodi ya matangazo ya pekee kwa ajili ya mitandao ya redio ya nchi za Amerika ya Latini, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York.

Kwa miongo kadhaa, sauti maarufu kama Edward R. Murrow, Marlon Brando, Audrey Hepburn na Frank Sinatra zilisaidia kusimulia simulizi za kimataifa, huku wasikilizaji wakisikiliza hotuba za kihistoria kutoka kwa viongozi kama John F. Kennedy, Mikhail Gorbachev, Nelson Mandela, Fidel Castro na Papa John Paul II.

Urithi huo umebadilika na kuwa UN News ya sasa,  jukwaa la vyombo vingi vya habari linalochapisha katika lugha 10 na kuunganisha hadhira katika zaidi ya nchi 170. Linaleta habari za dharura, mahojiano, matangazo ya moja kwa moja na simulizi za kina kuhusu changamoto kubwa zinazoikabili dunia na juhudi za kuzitatua.

Licha ya mageuzi ya kiteknolojia, kanuni moja imebaki thabiti, kutoa taarifa za kuaminika kwa watu wanaozihitaji zaidi, kupitia mifumo ya sauti inayounganisha urithi na ubunifu.

Kujenga upya matangazo ya Redio Gaza

Hakuna mahali ambapo dhamira hii ni ya dharura zaidi kuliko katika maeneo ya migogoro. Gaza, kabla ya Oktoba 7, 2023, ilikuwa na jumla ya vituo 23 vya redio vya ndani. Baada ya vita vilivyochochewa na mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel, vituo vyote vilisambaratika.

Hata hivyo, Rami Al Sharafi, mkurugenzi wa Zaman FM, anajaribu kurejesha matangazo  juhudi dhaifu lakini zenye dhamira katikati ya uharibifu mkubwa.

Mwanamume amesimama katika jengo lililoharibiwa huko Gaza, akiwa amezungukwa na mabomoko na mabomoko, akizungumza na kamera.

Mwanahabari Rami Al-Sharfi, ni mkurugenzi wa redio katika kituo cha redio cha ZMN 90.60 FM cha Gaza.

Alipozungumza na Idhaa ya Kiarabu ya UN News, amesema wazi: “Zaman FM imerejea hewani, na kwa sasa sisi ndio kituo pekee kinachorusha matangazo ya FM kutoka ndani ya Ukanda wa Gaza baada ya uharibifu huu mkubwa.”

Hitaji la utangazaji wa kuaminika ni kubwa, hasa wakati Gaza ikikabiliwa na kuenea kwa magonjwa, kuporomoka kwa mfumo wa elimu na kuvurugika kwa huduma za umma.

Mvulana mdogo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anashikilia redio ya zamani, inayowakilisha matangazo ya elimu wakati wa janga la COVID-19.

UNICEF DRC Dicko

Radio Okapi na Radio nationale congolaise wamejitolea kutangaza mfululizo wa mafunzo juu ya masomo kuu ya darasa la msingi na sekondari nchini DRC wakati wa janga la Covid-19

Chombo muhimu kwa ulinzi wa amani

Katika maeneo mengine ya migogoro, redio ni nguzo ya utulivu. Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Radio Okapi imekuwa sauti ya kuaminika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 kama sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO.

Ikirusha matangazo kwa Kifaransa na lugha nne za kitaifa, kituo hicho hutoa taarifa za kuaminika katika maeneo yaliyoathiriwa na vurugu na watu waliokimbia makazi yao.

Mkazi mmoja wa Bukavu amesema Radio Okapi “ina jukumu muhimu katika kukuza amani kwa kurusha taarifa za kuaminika na zisizoegemea upande wowote,” akiongeza kuwa “watu wanapotaka kuhakikisha habari ni za kweli, mara nyingi hukimbilia Radio Okapi.”

Mwanamke mwenye shati nyekundu anahoji mwanamke mchanga akiwa na kipaza sauti katika tukio la nje lililoandaliwa na Guira-FM, kituo cha redio cha Umoja wa Mataifa kinachoendeleza amani na upatanisho katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

UN/MINUSCA

Radio ni mkombozi hasa kwa jamii za wakimbizi ambao husaka taarifa muhimu.

Kwa wakimbizi kama Bahati Yohane, anayeishi sasa katika kambi ya Kyangwali nchini Uganda, redio ilikuwa uhai. “Kwa kweli kabisa, kama isingekuwepo redio Okapi ya kutueleza kuhusu usalama, tusingekuwa hai leo,” ameiambia Idhaa ya Kiswahii ya UN News.

Mashujaa wa mawasiliano wakati wa majanga

Nje ya maeneo ya vita, umuhimu wa redio hujitokeza zaidi wakati wa majanga ya tabianchi. Mawimbi ya redio mara nyingi hubaki kuwa njia ya mwisho ya mawasiliano pale simu na intaneti zinapokatika.

Jesús Miguel Sarmiento, aliyetambuliwa kama XE1EW, anatabasamu huku akiendesha kituo cha redio akiwa rais wa Shirikisho la Wataalamu wa Redio la Mexico.

Eloísa Farrera/CINU México

Jesús Miguel Sarmiento, XE1EW, anaongoza Shirikisho la Mexico la Majaribio ya Redio wakati wa hafla ya redio.

Nchini Mexico, waendeshaji wa redio za mawasiliano ya hiari walitambuliwa kama mashujaa wa kitaifa baada ya tetemeko la ardhi la mwaka 1985, wakati mifumo ya kawaida ya mawasiliano ilishindwa kabisa kufanya kazi.

Wakati wa Kimbunga Otis mwaka 2023, waliweza kubuni mifumo ya mawasiliano kwa haraka katika mazingira magumu. “Walibadilisha waya za shaba kuwa antena, wakatumia vifaa na betri zao, na mara moja wakaanza kurusha taarifa,” amesema Rais wa Shirikisho hilo, Jesús Miguel Sarmiento Montesinos.

Jukwaa la ujumuishaji

Redio pia ni chombo cha ujumuishaji. Nchini India, Radio Udaan ilianzishwa mwaka 2014 kama redio ya kwanza mtandaoni inayoendeshwa kikamilifu na watu wasioona. Leo inawafikia wasikilizaji 125,000 katika nchi 120.

media:entermedia_image:5bfda0f9-5771-4efe-945b-3c96c28595ad

© Radio Udaan

Kituo cha Redio cha Mtandaoni Kikitoa Sauti kwa watu wenye ulemavu wa kuona wa India.

Mwanzilishi Danish Mahajan anasema kuwa uzoefu wake binafsi humsaidia kuandaa vipindi vinavyokidhi mahitaji ya wasikilizaji. Amebainisha pia umuhimu wa maudhui ya UN News katika mijadala kuhusu haki za watu wenye ulemavu.

Anaona pia fursa mpya kupitia akili Mnemba (AI), akiielezea kama “teknolojia inayobadilisha mchezo kwa kuongeza ufikiaji kupitia vifaa kama miwani mahiri.”

Huruma Isiyoweza kuigwa na mashine

Akili Mnemba inabadilisha mazingira ya sauti duniani. Profesa Sun Shaojing wa Chuo Kikuu cha Fudan nchini China anaeleza kuwa watangazaji wa habari wanaozalishwa na AI wanazidi kuwa wa kawaida, wakitoa usahihi na ufanisi mkubwa.

Picha ya karibu ya roboti ya Ameca kwenye mkutano wa AI for Good Global Summit huko Geneva, Uswisi, na mtu akishikilia simu mahiri ili kupiga picha.

UN Photo/Elma Okic

Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Global Digital Compact unalenga kuunganisha serikali na viwanda ili kuhakikisha kwamba teknolojia, kama vile AI, inafanya kazi kwa ajili ya wanadamu wote.

Lakini akaonya kuwa sauti ya binadamu kusita, mapumziko na hisia ndizo zinazoipa sauti uhai wake. “Unaporipoti kuhusu maafa na mateso ya watu, AI itapoteza vipengele vya huruma na uhusiano wa kibinadamu,” amesema.

Mahitaji ya mawasiliano hata angani

Hata nje ya Dunia, redio ni msingi wa mawasiliano na utafiti. Tangu satelaiti ya kwanza kurushwa mwaka 1957, mawimbi ya redio yamekuwa daraja lisiloonekana la mawasiliano ya anga.

Alexandre Vallet wa Shirika la Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano ITU, amesema kuwa mipango ya kujenga vituo vya kudumu Mwezini inaweza kuongeza sana mahitaji ya mawasiliano ya redio.

“Katika mkutano ujao wa kanuni za redio mwaka 2027, tutajadili kwa mara ya kwanza mfumo wa kusimamia masafa ya redio Mwezini,” amesema.

media:entermedia_image:d628ddba-edca-47c9-9e7e-251b55270cdd

Setilaiti, kama inavyoonekana kutoka angani, inapita Amerika Kusini.

Mawimbi yanayodumu

Katika maeneo ya migogoro, majanga, juhudi za ujumuishaji na hata katika uchumi wa anga, redio inaendelea kuonesha nguvu yake ya kimya lakini ya ajabu.

Katika dunia inayozidi kufurika picha na teknolojia inayokimbia kwa kasi, mawimbi haya yasiyoonekana yanabaki kuwa ukumbusho kwamba njia rahisi zaidi za mawasiliano mara nyingi ndizo zenye nguvu kubwa zaidi kuhabarisha, kulinda na kuunganisha watu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *