
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa nchi tatu za Ulaya, yaani Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani, zimehusika katika uchochezi na machafuko ya karibuni dhidi ya Iran. Amesema kwamba, kwa mtazamo wa wananchi wa Iran, nchi hizo zimeshirikiana na watenda jinai wakuu katika machafuko hayo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran wiki hii alikuwa Hujjat al-Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari, katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini (MA).
Akiashiria vita vya kichokozi vya siku 12 vya Israel na Marekani dhidi ya Iran mwezi Juni mwaka jana, Hujjat al-Islam Haj Ali Akbari amesema kuwa, baada ya vita hivyo na kufuatia machafuko ya hivi karibuni, maadui walianzisha “operesheni nzito” dhidi ya wananchi wa Iran katika fremu ya vita vya kisaikolojia na propaganda.
Amesema operesheni hiyo ilihusisha, miongoni mwa mambo mengine, takwimu za uongo, madai ya kupotosha, simulizi zisizo za kweli kwa kutumia watu maarufu wakiwemo wasanii na wanamichezo pamoja na shinikizo kwa wafanyabiashara na makundi ya kijamii. Ameongeza kuwa kulikuwa pia na shinikizo la kimataifa, vikwazo vinavyojirudia, na maonesho ya kisiasa ya nchi za Ulaya ambazo ni vibaraka.
Khatibu huyo wa Ijumaa amesisitiza kuwa nchi hizo za Ulaya, hasa Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani, zimeshiriki katika uhasama dhidi ya Iran, iwe ni katika vita vya siku 12 au “fitna ya Kizayuni” ya hivi karibuni ambayo wachochezi wake wakuu walikuwa pia ni Marekani na Israel.
Hujjat al-Islam Haj Ali Akbari, pia ameashiria ushiriki mkubwa na wenye maana wa wananchi katika maandamano ya tarehe 11 Februari na kusema, baada ya vita vya siku 12 na fitna za karibuni, kwa kuhudhuria kwa mamilioni katika ulingo wa umma, taifa la Iran limebadilisha hesabu za adui na likaonesha ulimwenguni uwezo wa kuzuia na kujilinda.
Katika sehemu nyingine ya khutba zake, Hujjat al-Islam Haj Ali Akbari amewakumbusha waumini kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unakaribia. Kwa msingi huo amewataka Waislamu kujiandaa kwa mwezi huo mtukufu, aliouelezea kuwa ni mwezi bora zaidi katika miezi ya Mwenyezi Mungu, ambamo waumini wanaalikwa kwenye dhifa ya Mola wao.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na mpango wa kiroho kabla ya kuingia Ramadhani, akihimiza maandalizi yanayozingatia maelekezo ya Ahlul Bayt (AS), ili kuuingia mwezi huo kwa maisha yenye kujisitiri, utakaso wa akili na fikra, usafishaji wa nyoyo, na kuimarisha uhusiano wa kiroho baina ya mja na Mwenyezi Mungu.