
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa, Imam Hussein (a.s.) ametufundisha kusimama dhidi ya dhulma, vishawishi vya madaraka, na tamaa ya maslahi binafsi.
Rais Masopud Pezeshkian amesema hayo katika andiko lake kwenye mtandao wa kijamii kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Ashura ya Imam Hussein na kubainisha kwamba, “Ama baad; dunia ni kana kwamba haijawahi kuwepo kabisa, na akhera ni kana kwamba imekuwepo daima.
Pezeshkian aliongeza: Imam Hussein (a.s.) ametufundisha kusimama dhidi ya dhulma, vishawishi vya madaraka na tamaa ya maslahi binafsi; inawezekana kutoa uhai, lakini si heshima ya uhuru na utu; inawezekana kubaki peke yako, lakini si kuacha ukweli. Tusitende dhulma, tusikubali dhulma, na tusinyamaze mbele yake.
Wakati huo huo, mamilioni ya Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maeneo mengine ya dunia leo wameshiriki katika maombolezo ya kumbukumbu ya Ashura ya kukumbuka siku ya kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (a.s).
Ashura ni mwezi 10 Mfunguo Nne, Muharram, ambayo mwaka huu imesadifiana na leo Alkhamisi 25 Juni, 2026.
Imam Husain AS aliuawa shahidi kikatili mwaka wa 61 Hijria katika jangwa la Karbala nchini Iraq baada ya kuongoza mapambano ya kishujaa ya ushindi wa damu mbele ya upanga.
Waombolezaji hapa nchini Iran wakiwa wamevaa nguo nyeusi, kama ishara ya huzuni na majonzi, walikuwa wakibubujikwa na machozi kwa kukumbuka dhulma iliyofanywa na madhalimu dhidi ya kizazi bora cha Mtume Muhammad (saw).