Dar es Salaam. Imesalia takribani miezi miwili kabla ya kutimia miaka 10 tangu staa wa Bongofleva, Rayvanny, (32), kutoka rasmi kimuziki mara baada ya kutambulishwa na WCB Wasafi akiwa kama msanii wa pili wa lebo hiyo.

Umaarufu wa jina lake na kuanza kujitambulisha kama chapa, vilikuja kupitia wimbo wake, Kwetu (2016) uliotayarishwa na Laizer Classic chini ya Wasafi Records.

Video yake ambayo iliachiwa Aprili 14, 2016, ilishutiwa Dar es Salaam chini ya usimamizi wa Godfather Production kutokea Afrika Kusini, na kilichofuata baada ya hapo ni historia.

Hadi sasa hiyo ndio video ya wimbo wa Rayvanny alioimba pekee yake (solo) ambayo imefanya vizuri zaidi YouTube ikiwa imetazamwa zaidi mara milioni 45. Pia ilikamata nafasi ya sita Tanzania kwa kutazamwa zaidi 2016.

Video hiyo ina historia kubwa kwa Rayvanny kwani huo ndio mradi wa kwanza kufanya na mpenzi wake, Fahyma ambaye ana rekodi ya kipekee kwake.

Ikumbukwe Fahyma, mwanamitindo aliyeshinda tuzo kibao za kimataifa, ndiye mrembo aliyotokea mara nyingi zaidi katika video za Rayvanny.

VA 01

Ukiachana na Kwetu (2016), Fahyma amezipamba video za Rayvanny nyingine kama Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023). 

Kufanya vizuri kwa nyimbo zake mbili za mwanzo (Kwetu na Natafuta Kiki – 2016), kulichangia Rayvanny kuchaguliwa kuwania tuzo kama Africa Entertainment Awards, USA (AEAUSA), na MTV MAMAs 2016.

Baadaye akaja kushinda tuzo ya BET 2017 huko Marekani, kisha zikafuata nyingine kama Zikomo (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA (Kenya) 2022, DIAFA (Dubai) 2022 n.k.

Katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) ambazo zilirejea mwaka 2022 baada ya kusimama tangu 2015, huku Rayvanny ameshinda mara mbili kupitia nyimbo zake, Nitongoze (2022) na Kitu Kizito (2023). 

VA 02

Baada ya takribani miaka sita ya kufanya kazi pamoja tena kwa mafanikio makubwa, Rayvanny aliachana na WCB Wasafi akiwa tayari ameanzisha lebo yake, Next Level Music (NLM).

Utakumbuka chini ya usimamizi wa WCB Wasafi, aliachia Extended Playlist (EP) tatu, Flowers (2020), New Chui (2021) na Flowers II (2022), pamoja na albamu moja, Sound From Africa (2021).

Na baada ya kuondoka WCB Wasafi ametoa EP moja, Unplugged Session (2022) na albamu moja, The Big One (2024) yenye nyimbo 18, miradi yote hii ikisimamiwa na lebo yake, NLM.

VA 03

Lebo ya NLM ilitambulishwa rasmi Aprili 2021, na kufikia Septemba 2021, ikamtambulisha msanii wake kwanza, Mac Voice aliyekuja na EP yake, My Voice EP (2021) yenye nyimbo tano.

Hata hivyo, kwa sasa Mac Voice hayupo tena NLM na hasikiki kabisa kimuziki, hadi anaachana na lebo hiyo kimya kimya, alikuwa amefanya kolabo tano na Rayvanny ambazo zilimtangaza vizuri. 

Nyimbo hizo ni Tamu (2021), Bora Peke Yangu (2021), Pombe (2021), Muongeze (2022) na Mwambieni (2023).

Januari 2025, video ya wimbo wake, Number One (2020) akimshirikisha Zuchu, ikaweka rekodi ya kutazamwa mara milioni 100 YouTube ikiwa ni video yake ya kwanza, na hadi sasa hamna nyingine iliyofanya hivyo.

VA 04

Kwa matokeo hayo, aliungana na Diamond Platnumz, Harmonize, Zuchu na Jux katika orodha ya wasanii wa Bongofleva ambao wamefanikiwa kuwa na video moja au zaidi zilizofikia namba hizo.

Septemba 2025, Rayvanny akawa msanii wa pili Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa kazi zake kutazamwa (views) mara bilioni 1 YouTube akiwa amemfuatia Diamond.

Hata hivyo, huwezi kuzungumzia hatua hii kubwa bila kutaja mchango wa Diamond ambaye amekubali kushiriki katika nyimbo nane za Rayvanny kati ya 10 walizoshirikiana hadi sasa.

Ngoma za Rayvanny ambazo Diamond kasikika ni Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020), Woza (2020), Nitongoze (2022), Yaya (2023) na Nesa Nesa (2024).

VA 05

Katika miaka hii 10, wimbo wake unaotajwa kuwa na mafanikio makubwa zaidi ni Tetema (2019) akiwa na Diamond, huku S2kizzy akisimama upande wa utayarishaji.

Ndio wimbo wake pekee uliopata kuwa na remix nyingi ambazo ni nne, huku zikihusisha wasanii mbalimbali wakubwa duniani.

Mmoja wapo ni Maluma ambaye remix yake iliitwa ‘Mama Tetema’ akiwa na Rayvanny, na ilijumuishwa katika albamu, Don Juan (2023) ambayo iliwania tuzo za 66 za Grammy 2024 katika kipengele cha Best Latin Pop Album.

Novemba 2021, Rayvanny aliandika rekodi kama msanii wa kwanza kutoka Afrika kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs), ambapo alishirikiana na Maluma kutokea Colombia. 

Kumbuka pia huyu ni msanii wa kwanza Tanzania kushika namba moja chati za Billboard Mexico Airplay kupitia wimbo, Mama Tetema (2021). Pia alishafanya hivyo katika Billboard Top Triller Global Chart akiwa na Dj Cuppy wa Nigeria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *