DAR ES SALAAM: Wizara ya Madini imefanya mazungumzo ya kimkakati na World Gold Council (WGC) kwa lengo la kujadili namna baraza hilo litakavyoweza kuisaidia Tanzania kuvutia uwekezaji zaidi, hususan katika eneo la uongezaji thamani wa madini yanayopatikana nchini.

Mazungumzo hayo yameongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, kwa kushirikiana na Mawaziri wa kisekta, ambapo walikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa WGC, David Tait.

Katika kikao hicho, Serikali ilisisitiza msimamo wake wa kutokubali kusafirisha dhahabu ghafi nje ya nchi, ikieleza kuwa mkakati huo unalenga kuvutia uwekezaji katika viwanda vya kusafisha na kutengeneza bidhaa za dhahabu hapa nchini. Hatua hiyo inalenga kuongeza ajira, mapato ya ndani na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.

Pande zote pia zilijadili kwa kina namna ya kukuza sekta ya dhahabu ili iweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya nchi. Kipaumbele kiliwekwa katika urasimishaji na uwezeshaji wa wachimbaji wadogo, ambao wanachangia takribani asilimia 40 ya uzalishaji wa dhahabu nchini. Serikali imeeleza mpango wake wa kuwawezesha wachimbaji hao kufanya kazi kwa tija, kwa kuzingatia kanuni za usalama, utunzaji wa mazingira na uendeshaji wa kisasa.

Aidha, WGC imeonesha kuvutiwa na mfumo wa Tanzania wa usimamizi wa sekta ya madini na kuichagua nchi hiyo kwa ushirikiano maalum wa kukuza sekta ya dhahabu. Kupitia ushirikiano huo, baraza hilo litasaidia kuwajengea uwezo, maarifa na teknolojia wachimbaji wadogo ili Tanzania iweze kuwa kitovu (hub) cha mfano wa maendeleo ya sekta ya dhahabu barani Afrika.

Kutokana na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika, WGC imeeleza utayari wake wa kushirikiana na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuwainua wachimbaji wadogo, ambao licha ya mchango wao mkubwa, bado wanakabiliwa na changamoto za vifaa duni, ukosefu wa taarifa za kijiolojia na ugumu wa kupata mikopo kwa ajili ya mitaji.

Mawaziri wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka; pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *