
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 13, 2026 katika mji mkuu wa Antananarivo, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini humo, Tania Goossens, ameeleza kuwa watu wapatao 400,000 wanakabiliwa na mahitaji makubwa ya kibinadamu baada ya nchi hiyo kupigwa na vimbunga viwili ndani ya wiki tatu pekee.
Uharibifu huo ni wa kutisha, huku mji wa Toamasina ukiwa na asilimia tano tu ya umeme kwa sasa na kukosekana kwa huduma za maji safi. Goossens ameeleza hali aliyoiona baada ya kimbunga hicho
“Kiwango cha uharibifu ni kikubwa mno… Niliona familia zikijaribu kuokoa vitu vichache vilivyobaki kwenye nyumba zao. Wengi wanakesha usiku kwenye nyumba ambazo paa zimeezuliwa”, ameeleza.
Afya na maisha ya wananchi viko mashakani
Mamlaka nchini Madagascar zimeripoti vifo vya watu 38 na wengine 374 kujeruhiwa, huku shule, biashara, na hospitali ya mji huo zikiharibiwa vibaya. Mbali na njaa, kuna hofu kubwa ya kuzuka kwa magonjwa kutokana na ukosefu wa maji safi na miundombinu ya usafi iliyoharibiwa. Familia nyingi zimepoteza kila kitu na hazina uhakika wa kupata mlo unaofuata, huku barabara zikiwa zimefungwa na miti iliyoanguka na uchafu uliotapakaa mji mzima.
Kwa sasa, WFP inatumia akiba yake ya mwisho ya chakula kugawa kwa wahanga, lakini mahitaji ni makubwa kuliko uwezo wa shirika hilo. Kabla ya vimbunga hivi, tayari watu milioni 1.57 nchini Madagascar walikuwa na uhaba wa chakula, na sasa hali imekuwa mbaya zaidi. Tania Goossens amesisitiza uhitaji wa msaada wa haraka.
“Familia zinatuambia kuwa zimepoteza kila kitu… Wengi wamehifadhiwa kwenye nyumba zilizoharibiwa au kambi za muda na hawajui watapataje mlo unaofuata”, amesema.
Madagascar inahitaji msaada wa haraka wa dola milioni 18 ili kukabiliana na njaa katika kipindi cha miezi sita ijayo. Kwa kuwa huu ni mwanzo tu wa msimu wa vimbunga, kuna hofu kuwa majanga zaidi yanaweza kutokea huko mbeleni.